" Marekani Yagundua Mabilioni ya Pesa Kuibiwa na Kusafishwa Kenya Kinyemela

Marekani Yagundua Mabilioni ya Pesa Kuibiwa na Kusafishwa Kenya Kinyemela

 

Mamlaka za Polisi wa Shirikisho za Marekani, zimebaini udanganyifu mkubwa wa kifedha katika programu mbalimbali za Serikali ya jimbo la Minnesota, ambapo kiasi cha takribani Shilingi Bilioni 32.3 za Kenya (sawa na Mamia ya Mamilioni ya dola za Marekani), zimeibwa.

Kwa mujibu wa taarifa za waendesha Mashtaka wa Marekani, fedha hizo zilipatikana kupitia madai ya uongo na matumizi mabaya ya programu za Serikali, zikiwemo zile za misaada ya kijamii, chakula, na huduma za kijamii, ambazo zilikuwa zinalenga kusaidia wananchi wenye uhitaji mkubwa.

Uchunguzi umebaini kuwa sehemu ya fedha zilizoibwa zilisafirishwa nje ya Marekani na kisha kusafishwa kupitia uwekezaji katika sekta ya mali isiyohamishika nchini Kenya, ikiwemo ununuzi wa Majengo, Ardhi, na Miradi ya Maendeleo katika maeneo mbalimbali, hasa mijini.

Maafisa wa Marekani wamesema mbinu za kificho zilitumika kuficha chanzo cha fedha hizo, zikiwemo matumizi ya akaunti nyingi za benki, Kampuni hewa, na watu wa kati, hatua iliyolenga kuzuia Mamlaka za fedha kugundua uhalifu huo mapema.

Hadi sasa, watu kadhaa wamefunguliwa Mashtaka kwa makosa ya kula njama, utakatishaji fedha, udanganyifu wa kimtandao, na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Uchunguzi bado unaendelea huku Mamlaka za Marekani zikishirikiana na taasisi za kimataifa kufuatilia mali zilizonunuliwa nje ya nchi na kurejesha fedha zilizoibwa.

Serikali ya Marekani imesisitiza kuwa haitavumilia matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi na imeahidi kuimarisha mifumo ya usimamizi na uwajibikaji ili kuzuia udanganyifu wa aina hii siku zijazo.

Kwa upande mwingine, wachambuzi wanasema madai ya fedha kusafishwa kupitia sekta ya mali isiyohamishika nchini Kenya yanaonyesha haja ya kuimarishwa kwa ushirikiano wa Kimataifa katika kupambana na uhalifu wa kifedha na kuhakikisha mifumo ya kifedha inalindwa dhidi ya matumizi haramu.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post