" PINDA ALAANI VURUGU ZA OKTOBA 29: ASEMA HAYAKUWA MAANDAMANO BALI NI MPANGO WA KUHUJUMU TAIFA

PINDA ALAANI VURUGU ZA OKTOBA 29: ASEMA HAYAKUWA MAANDAMANO BALI NI MPANGO WA KUHUJUMU TAIFA

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda atoa ujumbe mzito wa Mwaka Mpya akiitaka jamii kulinda uzalendo huku Serikali mkoani Katavi ikitaja mapinduzi ya miundombinu kama jibu la maendeleo kwa wananchi

Waziri Mkuu huyo Mstaafu wa Awamu ya Nne akilaanii machafuko hayo yaliyotokea Oktoba 29,2025 alisema wazi kuwa yale hayakuwa maandamano ya amani kama yalivyodhaniwa na wengi. 

Akizungumza kwa uchungu na msisitizo wa kizalendo wakati wa sherehe za Mwaka Mpya zilizofanyika katika Shule ya Sekondari ya Mizengo Pinda iliyopo Kibaoni mkoani Katavi, mzee Pinda amefafanua kuwa kundi la vijana lilishiriki  mipango ya makusudi ya kuharibu mali za watu, miundombinu ya umma na kutaka kuvuruga amani ya nchi ambayo ndiyo hazina kuu ya Watanzania. 

Waziri Mkuu huyo mstaafu ameweka wazi kuwa vitendo hivyo ni kinyume na ustaarabu wa taifa hili na ameitaka jamii kurejea katika misingi ya malezi bora ili kujenga vijana waadilifu na wazalendo ambao hawawezi kutumiwa kama nyenzo ya kuligawanya taifa au kubomoa kile kilichojengwa kwa jasho na damu.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na ndugu jamaa marafiki pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali mzee Pinda ametumia fursa hiyo kutoa onyo kwa wazazi na walezi akisisitiza kuwa jukumu la kuliokoa taifa dhidi ya machafuko ya baadaye linaanzia kwenye ngazi ya familia. 

Amesema kuwa vijana waliostaarabika hawawezi kushawishika kijinga kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu vinavyovika koti la maandamano ya amani na hivyo malezi ya kimaadili ni silaha pekee ya kulinda usalama wa nchi yetu kwa miaka ijayo. 

Ujumbe huo wa mzee Pinda umepokelewa na wageni waalikwa kama sauti ya busara inayolenga kuliponya na kuliunganisha taifa kufuatia makovu ya machafuko ya Oktoba 29,2025 huku kukiwa na msisitizo wa kudumisha umoja na utulivu uliopo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mlele Abdulmajid Mwanga akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi ameelezea juhudi za serikali katika kuibua fursa za kiuchumi kama njia ya kuwapunguzia wananchi kero na kuwafanya wawe na matumaini ya maendeleo badala ya kujiingiza kwenye vurugu. 

Mkuu huyo wa wilaya amebainisha kuwa serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Sitalike hadi Kibaoni kwa kiwango cha lami mradi ambao ulikuwa umekwama kwa miaka mingi na kusababisha adha kubwa kwa wasafiri na wafanyabiashara. Kukamilika kwa miundombinu hiyo ya barabara ni sehemu ya mikakati ya serikali ya awamu ya sita ya kufungua mkoa wa Katavi na kuhakikisha kuwa huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo zinaimarika ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Ujumbe uliotolewa katika hafla hiyo ya Mwaka Mpya nyumbani kwa mzee Pinda umetafsiriwa kama dira muhimu kwa Watanzania wote katika kuanza mwaka mpya kwa kutafakari thamani ya amani na madhara ya machafuko. 

Baadhi ya washiriki wa hafla hiyo wamesema kuwa maneno ya kiongozi huyo mstaafu yamejikita katika kurejesha mshikamano wa kitaifa na kuwakumbusha vijana kuwa maendeleo ya kweli hayaji kwa njia ya fujo bali kwa njia ya kufanya kazi na kulinda miundombinu inayojengwa na serikali. 

Hakika sauti ya mzee Pinda imesikika kama mbiu ya mgambo inayotaka kila mwananchi kuwa mlinzi wa amani ya mwenzake huku ikilaani kila aina ya jaribio la kutaka kurudisha nyuma hatua za kimaendeleo ambazo Tanzania imepiga hadi sasa.

 


Post a Comment

Previous Post Next Post