" SHAMRASHAMRA ZA MWAKA MPYA 2026: WATANZANIA WATHIBITISHA AMANI, WAKIIBEZA CHOKOCHOKO NA MAANDAMANO

SHAMRASHAMRA ZA MWAKA MPYA 2026: WATANZANIA WATHIBITISHA AMANI, WAKIIBEZA CHOKOCHOKO NA MAANDAMANO

Watanzania wameuanza mwaka mpya wa 2026 kwa kishindo cha furaha na amani ya kipekee ikiwa ni kielelezo cha wazi kuwa taifa hili ni kisiwa cha utulivu kisichoweza kutikiswa na chokochoko za kisiasa wala shinikizo la maandamano yasiyo na tija kupitia mitandao. 

Katika kila kona ya nchi kuanzia fukwe za Coco Beach jijini Dar es Salaam hadi viwanja vya Mwanga Community Center mkoani Kigoma na Nyerere Square jijini Dodoma wananchi wameonekana kuburudika kwa tabasamu na upendo wakidhihirisha ushindi dhidi ya mipango ya vurugu iliyokuwa ikipigiwa upatu hapo awali na watanzania wanaoishi na kula bata ughaibuni kupitia machafuko nchini Tanzania. 

Hatua hii ya wananchi kudharau na kubeza shinikizo la maandamano imetoa ujumbe mzito kuwa watanzania wa leo wanathamini amani kuliko mizozo na wameamua kushirikiana na serikali yao kuhakikisha hali inabaki kuwa shwari ili waendelee kufurahia matunda ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa nchi yao.

Serikali imedhamiria kwa dhati na inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kimsingi wa kulinda usalama wa raia na mali zao huku wananchi nao wakitekeleza wajibu wao wa kizalendo kwa kukataa kujiingiza katika mitego ya chuki na ukatili wa kisiasa mitandaoni. 

Taswira iliyojitokeza katika fukwe za Coco Beach inadhihirisha mshikamano wa hali ya juu ambapo wakazi wa Dar es Salaam na viunga vyake walijumuika kwa wingi pasipo hofu yoyote wakithibitisha kuwa Tanzania salama inasonga mbele kwa kasi ya ajabu. Hali kadhalika mkoani Mwanza na Kagera wananchi wameupokea mwaka kwa umoja na nidhamu huku wakazi wa Geita wakionyesha kuwa sehemu ya amani ya Tanzania kwa kuukaribisha mwaka mpya kwa utulivu uliopitiliza jambo linaloongeza imani kwa wawekezaji na watalii kuwa nchi hii ni sehemu salama zaidi duniani.

Ni vyema ikaeleweka kuwa amani tunayoiona si jambo la bahati mbaya bali ni matokeo ya utawala bora na umakini wa viongozi katika kusimamia haki na maslahi ya wote jambo ambalo limejenga imani kubwa kwa wananchi. 

Pamoja na furaha hiyo bado kuna haja ya kuimarisha maeneo ya starehe kama fukwe za Coco Beach kwa kuongeza mazingira ya kisasa ikiwemo maeneo ya watoto na huduma za mtandao ili kukuza zaidi utamaduni huu wa amani na utulivu. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuendelea kuwa mlinzi wa amani ya mwenzake na kuepuka ukatili wa kisiasa mitandaoni ambao unalenga kupandikiza chuki kati ya vijana wasanii na makundi mbalimbali ya kijamii kwani umoja wetu ndiyo fahari ya kizazi cha sasa na urithi wa vizazi vijavyo.

Kusherehekea mwaka mpya kwa amani kumezima kabisa sauti za wachache waliotaka kurudisha nyuma maendeleo ya taifa kupitia machafuko na badala yake kumeleta matumaini mapya ya ustawi wa jamii katika mwaka mzima wa 2026. 

Kwa utulivu huu wananchi wametoa onyo kwa wale wote wanaoendelea kupandikiza mbegu ya chuki mtandaoni kuwa watanzania wameshashtuka na hawatakuwa tayari kufuata mkumbo wa kuvunja amani kwa kisingizio chochote. 

Hakika mwaka huu uwe ni wa upendo na mshikamano ambapo kila tone la furaha lililoonekana katika sherehe hizi liwe ni chachu ya kufanya kazi kwa bidii huku tukilinda amani yetu ambayo ni ngao ya usalama na dira ya kuelekea Tanzania yenye mafanikio makubwa zaidi kimataifa.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post