Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amezuru eneo la ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro Januari 02 mwaka 2026 na kutoa agizo zito kwa Wizara ya Maji kuhakikisha mradi huo hausimami na unakamilika kwa wakati uliopangwa ili uanze kutoa huduma kwa wananchi.
Katika ziara hiyo Waziri Mkuu ameiagiza wizara husika kuandaa jedwali maalumu litakalokuwa mwongozo wa kasi kwa mkandarasi katika utekelezaji wa mradi huo huku akisisitiza kuwa ujenzi huu unaakisi maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji nchini.
Dkt. Mwigulu amebainisha kuwa Rais Samia ni kiongozi anayeona mbali kwani aliamua kutekeleza mradi huu wa kimkakati katika kipindi ambacho serikali inatekeleza miradi mingine mikubwa inayotumia fedha nyingi ikiwa ni hatua ya makusudi ya kutatua kero za Watanzania zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Akifafanua faida za mradi huo utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 366, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema kuwa kukamilika kwa bwawa hilo kutasaidia kuhifadhi lita bilioni 190 za maji zitakazokuwa mkombozi mkubwa wakati wa ukame pale kina cha Mto Ruvu kinapopungua.
Waziri Aweso ameongeza kuwa mbali na huduma ya maji mradi huo utazalisha takribani megawati 20 za umeme na utahusisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 72 hatua itakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Naye Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo amechombeza neema hiyo kwa kusema kuwa eneo kubwa linalozunguka bwawa hilo ni zuri kwa kilimo na wizara yake imejipanga kuwezesha kilimo cha umwagiliaji kwa mwaka mzima ili kukuza uzalishaji na malighafi za viwandani.
Safari hii ya miongo saba ya kiu na matumaini sasa inafikia tamati baada ya miaka mingi ya kusubiri huku kero ya mgao wa maji ikitesa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani .
Mradi huu wa kihistoria uliokuwa ndoto tangu miaka ya hamsini wakati wa serikali ya kikoloni sasa unatekelezwa kama alama ya ushindi dhidi ya changamoto za kimazingira zilizokuwa zimekwamisha mchakato huo kwa miaka mingi.
Kidunda itakuwa na uwezo wa kusambaza zaidi ya lita milioni 400 za maji kwa siku jambo litakalofanya kero ya mgao kubaki kuwa historia na kuleta utulivu kwa akina mama na familia zilizokuwa zikiteseka kutafuta huduma hiyo muhimu mjini na vijijini.
Mchanganuo wa mradi huu unaonyesha historia ndefu ambapo michoro ya awali na upembuzi yakinifu ulianza kufanyika zaidi katika miaka ya themanini kwa lengo la kudhibiti mafuriko na kutengeneza akiba ya maji ya kiangazi.
Mradi huu ulichelewa kwa miongo kadhaa kutokana na sababu kuu tatu ikiwemo mgogoro wa kimazingira na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu , sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kwani eneo la mradi linapakana na Pori la Akiba la Selous ambalo sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Sababu nyingine ilikuwa ni mabadiliko ya michoro mara kwa mara ili kuridhisha wadau wa mazingira pamoja na changamoto za kifedha ambazo sasa zimetatuliwa na serikali ya awamu ya sita iliyoamua kuupa mradi huu kipaumbele kwa fedha za ndani.
Shinikizo kubwa la kuhimiza kasi ya ujenzi hivi sasa linatokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha mto Ruvu kukauka mara kwa mara pamoja na ongezeko kubwa la watu na viwanda katika jiji la Dar es Salaam. Bila bwawa hili ukuaji wa viwanda na makazi unaathirika vibaya : na ndiyo maana agizo la Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba limekuja wakati muafaka kuzuia mradi usirudi tena kwenye usingizi wa miaka ya nyuma.
Hakika huu ni wakati wa neema ambapo kila tone la maji litakalotoka Kidunda litakuwa ni ushahidi wa kazi kubwa ya serikali katika kumkomboa mwananchi na kuliimarisha taifa kiuchumi na kijamii kwa viwango vya kimataifa huku kila upande ukijipanga kunufaika na uwekezaji huo wa Sh bilioni 366.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment