" Simba Kusajili Wachezaji Watatu wa Kigeni

Simba Kusajili Wachezaji Watatu wa Kigeni

 

DAR ES SALAAM:KLABU ya Simba SC imeendelea kuhusishwa na usajili wa wachezaji watatu wa kigeni katika dirisha hili la usajili, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha kikosi chake kuelekea michezo ya kimataifa na ya ndani.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya soka zinaeleza kuwa Wekundu wa Msimbazi wanamfuatilia kwa karibu winga wa kimataifa wa Senegal, Libasse Gueye, ambaye amekuwa akionesha kiwango kizuri katika ligi alikokuwa akicheza, huku kasi, uwezo wa kupiga chenga na kutengeneza nafasi vikitajwa kuwa miongoni mwa sifa zake kuu.

Mbali na Gueye, Simba pia inahusishwa na usajili wa Ndongani Gilbani, beki wa kati wa klabu ya Asante Kotoko ya Ghana, mchezaji anayesifika kwa uimara wa safu ya ulinzi, uzoefu wa mashindano ya Afrika you na uwezo wa kusoma mchezo kwa haraka.

Aidha, jina la Khadim Diaw, beki wa kushoto kutoka Mauritania, limekuwa likitajwa katika mipango ya Simba, ikielezwa kuwa uongozi wa klabu hiyo unatafuta kuimarisha upande wa kushoto wa ulinzi ili kuongeza ushindani na mbadala wa uhakika katika kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, licha ya taarifa hizo kuenea, Simba SC bado haijatoa tamko rasmi kuhusu kukamilika kwa usajili wa wachezaji hao, ikielezwa kuwa uongozi wake unasubiri kukamilisha taratibu zote muhimu kabla ya kuwatambulisha rasmi endapo makubaliano yatafikiwa.

Tayari Kocha Mkuu wa Simba Steven Barker alitoa taarifa kwa uongozi wa Simba kuwa anahitaji wachezaji watano wapya katika nafasi tofauti hivyo huenda utekelezaji umeanza kama hivyo.

Wakati sintofahamu za usajili zikiendelea, Simba tayari imeanza maandalizi kuelekea mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia, utakaochezwa nchini Tunisia wiki ijayo.

Post a Comment

Previous Post Next Post