
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew akizungumza katika Mkutano wa Waandishi wa Habari, Ikulu Jijini Dar es Salaam kuhusu Ziara ya Kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyofanya Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 12-15 Februari, 2026. Naibu Waziri Mhandisi Kundo alizungumzia kwa kina masuala mbalimbali yaliyojiri kwenye sekta ya maji pamoja na faida ambazo Tanzania imepata katika mkutano huo.
…………..
Na. John Bukuku – Dar es Salaam
Ulinzi, usalama na amani ni vitu vinavyokwenda sambamba na uchumi na biashara, ikisisitizwa kuwa pasipokuwa na utulivu hakuna biashara inayoweza kufanyika.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ameyasema hayo Februari 16, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akijibu swali la mwandishi wa habari Ally Mayala wa Magazeti ya Serikali (TSN) aliyetaka kufahamu, pamoja na mambo mengine, faida zinazoweza kupatikana kwa Tanzania kiuchumi, hasa katika soko la Afrika, kufuatia kuteuliwa katika nafasi za uongozi wa Umoja wa Afrika (AU), hususan uteuzi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na namna unavyoweza kuchagiza na kunufaisha uchumi wa nchi.
Akizungumzia uteuzi huo na mjadala mpana wa usalama barani Afrika wakati wa Mkutano wa 39 wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia, Balozi Kombo amesema kuwa ulinzi wa njia zote kuu za kibiashara unapaswa kupewa kipaumbele cha kipekee ili kuimarisha usalama wa uchumi wa bara la Afrika.
Amesema hatua hiyo itasaidia pia kupaza sauti katika masuala ya usalama, kupunguza gharama za bima na kuimarisha biashara, uwekezaji usafirishaji na utalii.
Balozi Kombo amebainisha kuwa masuala ya usalama yanaenda sambamba na uchumi, siasa na biashara za kimataifa, akifananisha hali ya usalama na “credit rating”, akieleza kuwa kadri hali ya usalama inavyokuwa nzuri ndivyo gharama za bima na mikopo zinavyopungua na fursa za kiuchumi kuongezeka.
“Usalama una mchango mkubwa katika uchumi wa nchi au bara. Kadri tunavyoimarisha usalama, ndivyo tunavyovutia uwekezaji, kupunguza gharama za biashara na kufungua fursa mpya za maendeleo,” amesisitiza.
Pia ameongeza kuwa, mbali na masuala ya usalama, kuna fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinahitaji muda kuzizungumzia kwa kina, akitolea mfano nchi ambazo awali hazikuwa na utulivu wa kutosha lakini zilipata mafanikio makubwa ya kiuchumi baada ya kuimarisha usalama na mifumo yao ya uchumi.
Akizungumzia fursa za kiuchumi, Mitaji na uwekezaji kwa Watanzania, amesema ni muhimu kujiamini na kutumia fursa zilizopo katika soko la dunia, hususan kwenye kilimo cha mazao yenye mahitaji makubwa kama parachichi, akibainisha kuwa mahitaji ya kimataifa ni makubwa kuliko uzalishaji wa ndani.
Amesisitiza kuwa uteuzi wa Rais Samia kuwa Makamu wa Pili wa Mwenyekiti wa AU katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja huo unaongeza nafasi ya Tanzania kushiriki kikamilifu katika mijadala na maamuzi muhimu yanayohusu mustakabali wa usalama na maendeleo ya bara la Afrika.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameteuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto (Maternal, Child and Reproductive Health). Tanzania pia imeteuliwa kuwa mwenyeji wa Makao Makuu ya Kituo cha Mafunzo ya Vijana kuhusu mazingira barani Afrika. Katika nafasi za uongozi wa Umoja wa Afrika (AU), Mwenyekiti wa sasa ni Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye; Makamu wa Kwanza ni João Lourenço, Rais wa Angola; na Makamu wa Pili ni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria Mkutano wa Waandishi wa Habari, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Februari, 2026 kuhusu Ziara za Kikazi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizofanya Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 12-15 Februari, 2026 pamoja na Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) tarehe 2-6 Februari, 2026. 

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment