Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Kanali Yahya Ramadhani Kido kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 09 Februari, 2026. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Balozi Waziri Rajab Salum kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 09 Februari, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Meja Jenerali Marco Elisha Gaguti kuwa Balozi, kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 09 Februari, 2026.

Viongozi wateule wakiapa Kiapo cha Maadili kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 09 Februari, 2026.
……………Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam. Akizungumza katika hafla hiyo, Rais amesema maendeleo ya Taifa yanahitaji mabadiliko ya vitendo katika utekelezaji, uwajibikaji wa haraka, na ulinganifu wa sera na mipango na kasi ya mahitaji pamoja na matarajio ya wananchi.
Rais Dkt. Samia amesema uteuzi na mabadiliko aliyoyafanya yanalenga kuimarisha ufanisi na uwajibikaji katika utendaji wa Serikali, pamoja na kuhakikisha kuwa upangaji wa sera na mipango unaendana moja kwa moja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati na kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.
Taarifa iliyotolewa na Bakari S. Machumu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema Aidha, amewapongeza viongozi walioapa kwa kuteuliwa kwa misingi ya uwezo, uzoefu na uadilifu, na kuwakumbusha umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kulinda kiapo walichoapa mbele ya Mungu, Taifa na wananchi.
Kwa Wakuu wa Mikoa ya Kagera na Mtwara, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa mikoa hiyo ni ya kimkakati kiuchumi na kiusalama, na amewataka kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama, Wakuu wa Wilaya pamoja na wadau wa maendeleo ili kuimarisha amani, utulivu na usalama katika maeneo yao.
Kuhusu muundo mpya wa utumishi katika Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Rais Dkt. Samia amesema mabadiliko hayo yanalenga kuoanisha upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya Serikali ili kuhakikisha sera na mipango ya Taifa inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ina matarajio makubwa kwa sekta binafsi, inayotarajiwa kuchangia takribani asilimia 70 ya lengo la uchumi wa dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2050, huku Serikali ikichangia takribani asilimia 22 kupitia kodi, na sehemu iliyobaki ikichangiwa na mashirika ya umma.
Ili kufanikisha hilo, amesisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi kuhakikisha sekta binafsi na uwekezaji vinawezeshwa, badala ya kuzuiwa kwa sababu za kisheria na kiutawala.
“Muondoe sheria za kukwaza maendeleo. Fungulieni milango wawekezaji,” amesisitiza Rais Dkt. Samia kwa viongozi wenye dhamana ya kuratibu utekelezaji wa Dira 2050.
Aidha, ameiagiza Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji kusimamia mikakati ya kufungua fursa zaidi za uwekezaji na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kwa lengo la kuchochea ajira, mapato na ukuaji wa uchumi.
kKatika sekta ya nishati na mazingira, Rais Dkt. Samia amesema Serikali inalenga kuongeza uzalishaji wa umeme hadi kufikia takribani megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo maji, jua, gesi na mafuta. Hatua hiyo inalenga kuimarisha ukuaji wa viwanda na uchumi kwa ujumla, sambamba na kusisitiza matumizi bora ya fursa za biashara ya hewa ukaa (carbon credit) ili kulinda na kuongeza mapato ya Taifa.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amewaelekeza viongozi wa sekta za viwanda, biashara, kilimo, mifugo na uvuvi kuvutia uwekezaji, kuongeza thamani ya mazao, kuimarisha usindikaji na kupanua masoko ya ndani na nje, akisisitiza kuwa sekta hizo ni mhimili muhimu wa ajira na mapato ya Taifa, hususan kwa vijana.
Akihitimisha, Rais Dkt. Samia amewataka viongozi wote kufanya kazi kwa misingi ya uadilifu, uwazi, uwajibikaji na uzalendo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 unahitaji uwajibikaji wa kila kiongozi, na kwamba Serikali itafuatilia kwa karibu utendaji wao.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment