Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Mbeya
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa tahadhari kali kufuatia kusambaa kwa picha na taarifa katika mitandao ya kijamii zikimuonesha mwanaume mmoja anayejinasibu kuhusika katika tukio la mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM tawi la Itumbi, marehemu Elia Richard Sambala (53), mkazi wa Kijiji cha Itumbi, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, (SACP) Benjamin Kuzaga katika akieleza kuwa madai yanayosambazwa mitandaoni si sahihi na yanapotosha ukweli wa tukio hilo.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, tukio hilo lilitokea Februari 11, 2026 majira ya saa 7 mchana katika Kijiji cha Itumbi, ambapo Elia Richard Sambala alikutwa shambani kwake akiwa amejeruhiwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na watu wasiojulikana.
Alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa matibabu.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia kikosi cha upelelezi wa makosa ya jinai kilianza msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili kuhusiana na mauaji hayo.
Upelelezi zaidi unaendelea ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wengine wa tukio hilo ambapo uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa maslahi katika eneo la uchimbaji wa madini ya dhahabu.
Inadaiwa kuwa mmoja wa wanafamilia alikodisha eneo hilo kwa wawekezaji raia wa China kwa ajili ya shughuli za uchimbaji bila kuwashirikisha ndugu wengine, hali iliyosababisha mvutano uliokuja kuzaa tukio hilo la kinyama.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limemuonya vikali mtu huyo anayejitambulisha kama kiongozi wa kikundi kinachojiita TFF (Tanzania Freedom Fighters) kuacha kuzungumzia jambo hilo kwa namna inayokwenda kinyume na uhalisia.
Polisi wameeleza kuwa mtu huyo anatumia mitandao ya kijamii kupotosha ukweli na kuhamasisha uhalifu dhidi ya taasisi, viongozi na wananchi.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea na juhudi za kumtafuta mtu huyo ili akamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Wakati huo huo, wananchi wametakiwa kupuuza taarifa zisizo rasmi na kuacha kusambaza ujumbe wa upotoshaji unaoweza kuhatarisha amani na usalama.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment