" MNEC MWASELELA APONGEZA UWT MBEYA KWA MRADI WA NYUMBA ZA KITEGA UCHUMI

MNEC MWASELELA APONGEZA UWT MBEYA KWA MRADI WA NYUMBA ZA KITEGA UCHUMI


Na Lydia Lugakila-Misalaba Media

Mbeya

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, amempongeza Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Mbeya, Bi. Edina Mwaigomole, pamoja na baraza lake kwa ujasiri na uthubutu wa kuanzisha na kuendeleza mradi wa ujenzi wa nyumba mbili za kitega uchumi za umoja huo mkoani Mbeya.

Mwaselela amesema kuwa kukamilika kwa nyumba hizo kutaleta faraja kubwa kwa wanawake wa UWT mara zitakapokamilika na kupata wapangaji.
Pongezi hizo alizitoa Februari 7, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba hizo.

Akizungumza kabla ya kushiriki kikao cha UWT Mkoa wa Mbeya kilichofanyika katika Ofisi za CCM Mkoa wa Mbeya, alisema kuwa Bi. Edina Mwaigomole alilikuta eneo hilo likiwa tupu alipokabidhiwa uongozi, lakini sasa tayari kuna mradi unaoonekana na unaoacha alama, jambo linaloonesha ujasiri na uthubutu wa kiongozi huyo.

Ameeleza kuwa uongozi bora hauonyeshwi kwa maneno bali kwa vitendo, hivyo akawapongeza viongozi wa baraza hilo kwa kazi kubwa wanayoifanya.

“Miaka mitano ya uenyekiti wako imekuwa ya nguvu, na nguvu hiyo inaonekana kumbuka uongozi ni kuacha alama nakupa tano, na niko tayari kuwaunga mkono,” alisema Mwaselela.

Aidha, ameahidi kukamilisha kazi zilizobaki katika ujenzi wa nyumba hizo, ikiwemo kupiga plasta na kufanya finishing, na baadaye kuzikabidhi zikiwa zimekamilika kabisa.

Akitoa shukrani kwa niaba ya UWT Wilaya ya Mbarali, Bi. Zabibu Nuroo, alimshukuru Mwaselela kwa msaada wake mkubwa katika mradi huo wa kitega uchumi, akisema wanajivunia kuwa na MNEC anayejali na kusaidia wanawake mara kwa mara.

Kwa upande wake mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mbeya, Bi. Edina Mwaigomole, amewashukuru wadau wote waliochangia na kuunga mkono mradi huo, huku akimpongeza Mwaselela kwa namna anavyogusa na kusaidia makundi mbalimbali ya jamii, ikiwemo wanawake, wajane, watu wenye ulemavu na makundi mengine.

Awali akisoma taarifa ya UWT Mkoa wa Mbeya kuhusu mradi huo, Katibu wa UWT Mkoa wa Mbeya, Bi. Agnes Bashemu, alisema ujenzi wa nyumba hizo ulianza Septemba 2021 na kwamba Mwaselela amekuwa mdau namba moja katika kufanikisha mradi huo.

Kikao hicho cha UWT Mkoa wa Mbeya kiliwakutanisha wanawake kutoka wilaya za Mbeya Vijijini, Mbeya Jiji, Kyela, Rungwe, Mbarali na Chunya.
mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mbeya, Bi. Edina Mwaigomole.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post