" MNEC NDELE MWASELELA AAPA KUMLINDA RAIS SAMIA AELEZA ALIVYOHESHIMISHA WANAWAKE NCHINI

MNEC NDELE MWASELELA AAPA KUMLINDA RAIS SAMIA AELEZA ALIVYOHESHIMISHA WANAWAKE NCHINI

 


Na Lydia Lugakila-Misalaba Media


Mbeya


Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, ameapa hadharani kuwa hayuko tayari kumuacha yeyote anayethubutu kubeza, kumdharau au kujaribu kumdondosha Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.


MNEC Mwaselela ametoa kauli hiyo Februari 7, 2026, mbele ya Baraza la Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Mkoa wa Mbeya, katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi za CCM Mkoa kiliwakutanisha wanawake kutoka wilaya za Chunya, Mbeya Mjini, Mbeya Vijijini, Kyela, Rungwe na Mbarali.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwaselela alisema kuwa Rais Samia ameweka alama kubwa katika historia ya Taifa, hususan kwa kuwaheshimisha na kuwainua wanawake, kwa kufungua wigo mpana wa ushiriki wao katika siasa, uongozi na uchumi wa Taifa.

Amesema umahiri, ujasiri na uhodari aliouonyesha Rais Samia katika kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki kwenye siasa za uchumi na ujenzi wa Taifa ni wa mfano, akitolea mfano kuongezeka kwa idadi ya madiwani wa kata Wanawake pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wabunge wanawake, idadi ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa uongozi wa kisasa nchini.

“Tuna Rais wa mfano amewatendea haki wanawake, amehakikisha wanashiriki kikamilifu, si kwa jina tu bali kwa vitendo ambapo Wanawake leo wanakaa, wanapanga na wanajadili mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu,” alisema Mwaselela.

Ameongeza kuwa ni fahari kubwa kujenga na kudumisha mahusiano mema na viongozi wanaothamini haki, akisisitiza kuwa kila anapopanda jukwaa, yuko tayari kumsimamia na kumtetea Dkt. Samia bila kusita.

Mwaselela ameeleza wazi kuwa hatamvumilia mtu yeyote atakayethubutu kumdharau Rais Samia, akiahidi kuwa kama MNEC, mwanachama wa kawaida wa CCM na kijana, yuko tayari kumtetea Rais huyo hadharani yaani usiku na mchana.

“Kumtetea Rais Samia hakuhitaji fedha, hakuhitaji bei bali kunahitaji uzima na sauti" alisema Mnec huyo.

Ameongeza kuwa yupo Mwenyezi Mungu, halafu yupo Rais Samia na kwamba yeye ana jambo la kusema mbele ya Mungu kuhusu Rais Samia,” alisisitiza.

Aidha, amesema Rais Samia ameonesha upendeleo wa maendeleo kwa Mkoa wa Mbeya kwa kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii, jambo linalowapa wananchi wajibu wa kulinda maslahi mapana ya chama na uongozi wa Taifa, hasa kwa kuhakikisha Mwenyekiti wao wa Taifa anaendelea kuwa salama na kutekeleza majukumu yake kwa amani na utulivu.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post