" MWENYEKITI WILAYA YA MBEYA AANZA RASMI NA MIPANGO MIPYA YA MAENDELEO AAHIDI KUFANYA KAZI USIKU NA MCHANA

MWENYEKITI WILAYA YA MBEYA AANZA RASMI NA MIPANGO MIPYA YA MAENDELEO AAHIDI KUFANYA KAZI USIKU NA MCHANA

Na Lydia Lugakila-Misalaba media MbeyaMwenyekiti mpya wa Wilaya ya Mbeya kutoka Kanisa la Moravian, Mchungaji Greenwell Dickson Sinkwembe, ameahidi kufanya kazi usiku na mchana kwa kushirikiana na waumini na viongozi wenzake ili kuanzisha mipango na mikakati mipya itakayoboresha maisha ya Wakristo mmoja mmoja pamoja na kulijenga kanisa kiuchumi.Mchungaji Sinkwembe alitoa kauli hiyo Februari 15,2026 katika ibada maalum ya kumpokea rasmi kama Mwenyekiti wa Wilaya ya Mbeya, iliyofanyika katika Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Magharibi, Hosteli ya Ushirika wa Mabatini mkoani Mbeya.Amesema kuwa kwa sasa Wilaya ya Mbeya haina ofisi zake rasmi, hivyo inalazimika kutumia kwa muda ofisi za Kadege kwa makubaliano ya kuazima ambapo kutokana na hali hiyo, ameweka wazi azma ya kuanzisha mipango madhubuti ya kutafuta viwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za wilaya pamoja na nyumba za watumishi.Aidha, amewaomba Wakristo wa Wilaya ya Mbeya, wachungaji wenzake pamoja na mabaraza ya wazee wa mashirika yote kushirikiana kwa dhati ili kuhakikisha mipango ya maendeleo inaanza kutekelezwa mara moja.“Mshikamano na umoja ni vitu muhimu sana hivyo hatutafeli kwani tupo tayari kufanya kazi usiku na mchana ili tutoke tulipo,” alisema Mchungaji Sinkwembe.Ameongeza kuwa wako tayari kutumia nguvu, akili na hata mali zao ili kufanikisha malengo waliyojiwekea kwa maendeleo ya wilaya hiyo.Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa kuwahamasisha Wakristo kuwajibika katika utoaji wa sadaka na kuchangia mipango ya maendeleo itakayowasilishwa na Halmashauri ya Wilaya.Mtumishi huyo pia amewaonya waumini kutoruhusu vikwazo au migogoro kuathiri ushirika, akieleza kuwa amani ni msingi wa maendeleo.“Tusiruhusu migogoro, maana haijengi wala haileti mafanikio amani ndiyo nguzo ya maendeleo ya kanisa,” alisisitiza.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wilaya ya Uyole, Mchungaji Godfrey Tinga, amesema ana imani kubwa na uwezo wa Mchungaji Sinkwembe kutokana na uzoefu wake katika utumishi. Hata hivyo, Mchungaji Tinga amemtaka mchungaji Sinkwembe kuchapa kazi ya Mungu bila hofu wala kukata tamaa.Ibada hiyo imeashiria mwanzo mpya wa uongozi katika Wilaya ya Mbeya, huku waumini wakionesha matumaini makubwa ya kuona mabadiliko chanya na maendeleo endelevu ndani ya kanisa hilo.

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



 

Post a Comment

Previous Post Next Post