Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameteuliwa rasmi kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto (Maternal, Child and Reproductive Health).
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, uteuzi huo umeidhinishwa katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU uliofanyika tarehe 14 Februari 2026, jijini Addis Ababa, kufuatia mapendekezo ya Ripoti ya mwaka 2025 ya Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Africa Centres for Disease Control and Prevention (Africa CDC).
Machumu amesema kuwa katika wadhifa huo wa mwaka mmoja, Rais Dkt. Samia ataongoza juhudi za kuimarisha mshikamano na hatua za pamoja miongoni mwa nchi wanachama wa AU katika kuboresha afya ya uzazi pamoja na afya ya mama na mtoto barani Afrika.
Ameeleza kuwa lengo kuu ni kuhamasisha na kuongeza uwekezaji endelevu wa nchi wanachama katika sekta ya afya, kwa kutambua kuwa afya bora ya mama na mtoto ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na nguzo muhimu ya utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Afrika.
Aidha, Machumu amebainisha kuwa Rais Dkt. Samia atahamasisha uongozi wa kisiasa wa ngazi za juu katika nchi wanachama kubuni, kutekeleza na kufuatilia sera, mikakati na programu za Afya ya Uzazi na Haki za Uzazi (SRHR), huku msisitizo ukiwekwa katika kuhakikisha ahadi zinazotolewa kwenye mikutano ya kikanda na kimataifa zinageuzwa kuwa vitendo vyenye matokeo yanayopimika.
“Vilevile, atabeba jukumu la kukuza mfumo wa kujifunza na kushirikishana uzoefu baina ya nchi wanachama, ikiwemo kufanya tathmini za mara kwa mara za maendeleo yaliyofikiwa,” amesema Machumu.
Ameongeza kuwa utaratibu huo unalenga kusambaza mbinu bora, kubaini changamoto za pamoja na kuharakisha kufikiwa kwa malengo ya bara katika kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuimarisha huduma za afya ya uzazi.
Kadhalika, Rais Dkt. Samia atahamasisha ongezeko la uwekezaji kutoka serikalini, kwa washirika wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, kupunguza vifo na magonjwa yanayohusiana na afya ya uzazi ambayo huathiri zaidi wanawake, vijana na wasichana barani Afrika.
Kupitia nafasi hiyo, Machumu amesema Tanzania inaendelea kuonesha dhamira yake ya kuchangia uongozi wa bara la Afrika katika kujenga mifumo imara ya afya inayolinda haki ya kila mwanamke na mtoto kupata huduma bora za afya.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment