" RAIS SAMIA ATOA MAAGIZO KUHUSU SOKO JIPYA LA KARIAKOO

RAIS SAMIA ATOA MAAGIZO KUHUSU SOKO JIPYA LA KARIAKOO



Na. John Bukuku – Dar es Salaam

Rai imetolewa kwa wananchi na wafanyabiashara kulilinda, kulitunza na kulitumia kwa tija Soko Jipya la Kariakoo ili liendelee kuwahudumia wafanyabiashara wa leo na wa kesho wa ndani na nje ya nchi.

Rai hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Februari 08, 2026 wakati akizindua soko hilo lililopo Ilala jijini Dar es Salaam.

Amesema wafanyabiashara watakaopata fursa ya kutumia soko hilo wanapaswa kuwa walinzi wa wenzao kwa kuwa kuharibu soko ni kuchoma fedha za wananchi zilizotumika kujenga miundombinu hiyo na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi. Aidha, amebainisha kuwa ni jukumu la kila mmoja kulinda mali za umma na kudumisha amani popote alipo, huku akieleza matumaini yake kuwa soko hilo litakuwa mfano wa masoko ya kisasa barani Afrika na kitovu cha ustawi wa wananchi kiuchumi.

Akizungumzia vijana, amesema anatambua juhudi zao za kujitafutia kipato kupitia biashara ndogondogo na kuongeza kuwa kipaumbele cha Serikali ni kurasimisha biashara hizo hasa za vijana kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi ya mwaka 2025. Aidha, amebainisha kuwa Halmashauri zinapaswa kuweka miundombinu rafiki ya kufanya biashara kwa vijana ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na kuongeza kuwa Wakuu wa Wilaya wahakikishe utekelezaji wa agizo hilo pamoja na kuongeza asilimia 10% inayotolewa kwa vijana na wanawake kufikia asilimia 15% ili kuwajengea miundombinu ya kufanyia biashara.

Rais Samia amesema kuwa soko hilo haliwezi kuendeshwa kwa mfumo wa kizamani bali linahitaji mageuzi ya kiutawala, mtazamo na usimamizi unaozingatia huduma bora, nidhamu na ufanisi. Aidha, amebainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI inapaswa kulisimamia kwa ufanisi mkubwa.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuwa uamuzi wa Rais Samia wa ujenzi wa soko hilo ni ishara ya dhati ya kujitoa kwake kwa Watanzania hususan wafanyabiashara wa Kariakoo na watumiaji wa soko hilo. Aidha, amebainisha kuwa Rais Samia ameendelea kurejesha tabasamu kwa wananchi kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi anazozitoa jambo linalodhihirisha uongozi wake wa vitendo unaojali maslahi ya watu.

Ameongeza kuwa soko hilo limejengwa kwa misingi ya kisasa kwa kuzingatia maono ya Rais Samia ili kuhakikisha mazingira salama na rafiki kwa wafanyabiashara na pia amebainisha kuwa limewekewa mifumo imara ya umeme, kamera za ulinzi pamoja na jenereta za dharura kwa lengo la kuongeza usalama na ufanisi wa shughuli za biashara. Aidha amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na kukuza uchumi wa wananchi kupitia miundombinu ya kisasa na endelevu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema kuwa mkoa huo kwa pamoja wamekubaliana kufungua barabara zote za Kariakoo ili kuhakikisha eneo hilo halisimami kwa maendeleo kwa kuwa ni eneo muhimu kikodi na ni mkoa rasmi wa kikodi wa Mamlaka ya Mapato TRA.

Aidha, amebainisha kuwa tayari kupitia Shirika la Nyumba NHC kwa kushirikiana na wawekezaji binafsi yamejengwa majengo na kupatikana fremu za maduka zaidi ya 500 ili kuwapatia wafanyabiashara maeneo ya kufanyia biashara badala ya kufunga barabarani.

Ameongeza kuwa uzinduzi huo wa Soko Kuu la Kimataifa la Kariakoo na soko jipya umefanyika baada ya ukarabati na ujenzi mpya kufuatia ajali ya moto iliyotokea mwaka 2020. Aidha, amebainisha kuwa Rais Samia ametoa fedha za kutosha kujenga madaraja katika maeneo korofi kama Jangwani, Mwajuni na Kigogo ili kuhakikisha maeneo yote yanapitika wakati wa mvua.  


 


Post a Comment

Previous Post Next Post