Na. Joyce Ndunguru, Mara.
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Grumeti Reserve Ltd imekabidhi vifaa mbalimbali yakiwemo Madawati 3,015, Kompyuta 21, Vitanda vya hospital 24, UPS 8 pamoja na Printa 2 vyenye thamani ya takribani shilingi za kitanzania Milioni 362 kwa Wilaya za Serengeti na Bunda zilizopo Mkoani Mara.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano yaliyofanyika Februari 27,2026, Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi ambaye pia ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Kitengo cha Jamii, Utafiti na Ujirani Mwema, Omary Msangi alisema vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni utekelezaji wa Mkataba wa Uwekezaji Mahiri (SWICA) baina ya TAWA na Kampuni ya Grumeti Reserve Ltd kwa ajili ya shughuli za Uhifadhi katika Hifadhi za Ikorongo na Grumet.
Aidha , Kamishna Msangi aliongeza kuwa miongoni mwa matakwa ya Mkataba huo ni kuongeza mapato na kuhakikisha jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi hizo zinanufaika na uwepo wa rasilimali Wanyamapori katika maeneo yao.
Sambamba na hilo, Kamishna Msangi, alitoa rai kwa wananchi kuendelea kuunga mkono shughuli za uhifadhi na utalii zinazofanyika sehemu mbalimbali ili kuhakikisha kuwa manufaa yaliyoonekana leo yanaendelea kupatikana.
Naye, Kamanda wa Uhifadhi anayesimamia Kanda ya Ziwa, Mark Chuwa alisema TAWA imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika ulinzi wa maeneo ya hifadhi, Aidha, mashirikiano hayo pia yanajikita katika kuhakikisha wananchi wananufaika na rasimali za Taifa.
Kamanda Chuwa aliongeza kuwa vifaa hivi vilivyokabidhiwa vitaenda kupunguza changamoto za madawati zilizokuwepo katika mashule na kuboresha utendaji kazi katika Zahanati zinazopatikana katika Wilaya za Serengeti na Bunda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Mhe. Angelina Lubela aliwashukuru TAWA pamoja na Kampuni ya Grumeti kwa kuwakabidhi vifaa hivi ambavyo vitaenda kupunguza changamoto katika Sekta ya Elimu na Afya katika Wilaya ya Serengeti.
Pia, Mhe. Lubela aliongeza kuwa madawati haya yataenda kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi na kuwahamasisha wanafunzi kuhudhuria masomo yao hivyo kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Kaminyonge aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ambazo faida za wawekezaji hao zinagusa jamii moja kwa moja.
Kadhalika, Mhe.Kaminyonge aliishukuru TAWA pamoja na Kampuni ya Grumeti kwa vifaa hivyo yakiwemo madawati kwani yataenda kupunguza upungufu wa madawati kwa wanafunzi takribani 4,600 wa Wilaya ya Bunda.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Kampuni ya Grumeti Reserve Ltd, Frida Mollel alisema , Grumeti wataendelea kuhakikisha jamii zinazoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Ikorongo na Grumet wanafaidika na uwepo wao kama wawekezaji.
Aidha, alisema kuwa vifaa hivi vilivyotolewa kwa wananchi vikawe chachu katika kuendelea kuhamasisha wananchi kutunza maeneo ya hifadhi.
Post a Comment