Na Lydia Lugakila, Misalaba MediaMbeyaUmoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Mbeya umewakabidhi zawadi ya hati ya pongezi wabunge wawili wa viti maalum kutoka mkoani humo, Mhe. Suma Fyandomo na Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, ikiwa ni kutambua mchango wao, ushirikiano na kazi waliyoifanya ndani ya chama kwa kipindi cha miaka mitano.Zawadi hizo zilikabidhiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) kutoka Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, kwa niaba ya UWT Mkoa. Ofisi ya UWT Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Kamati ya Utekelezaji iliamua kuandaa zawadi hiyo maalum kwa ajili ya kuwapongeza wabunge hao kwa utumishi wao mzuri na kwa kuendelea kushirikiana vyema na wanawake wa UWT ndani ya chama na mkoa kwa ujumla.Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mbeya, Bi. Edina Mwaigomole, akizungumza kabla ya kutolewa kwa zawadi hizo alimpongeza Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya na naibu waziri wa maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, kwa kushiriki kikao cha UWT Mkoa wa Mbeya na kuendelea kuwa karibu na wanawake wa chama hicho.Akizungumza baada ya kupokea zawadi hiyo ya hati ya pongezi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amelishukuru Baraza la UWT Mkoa wa Mbeya kwa niaba yake na kwa niaba ya Mbunge mwenzake Mhe. Suma Fyandomo.Mhe Mahundi amesema zawadi hiyo ni faraja na motisha kubwa, kwani kutambuliwa kwa jitihada ulizozifanya mtu humtia mtu moyo wa kuendelea kupambana na kulitumikia Taifa au chama kwa bidii zaidi. Ameongeza kuwa UWT imeweza kutambua mchango wao kwa kipindi cha miaka mitano waliyoishi na kufanya kazi pamoja mkoani Mbeya, ambapo waliitumikia UWT kwa haki na uaminifu.Naibu waziri huyo amesisitiza kuwa katika shughuli zote wanazozifanya, lengo kubwa ni kuendelea kuimarisha UWT, kwani wanawake wakishaimarika, chama kitaimarika pia.Aidha ameeleza kuwa nafasi aliyompa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inawagusa moja kwa moja wanawake wa UWT, kwani wizara hiyo ni pana na inagusa maisha ya jamii kwa ujumla. Amefafanua kuwa wizara hiyo ni mtambuka na hufanya kazi kwa kushirikiana na wizara zote za kisekta ili kuhakikisha makundi ya wanawake yanashiriki kikamilifu katika fursa mbalimbali za maendeleo, ikiwemo kilimo cha kisasa ambacho kimewezeshwa na Serikali ya awamu ya Sita.Mhe Mahundi amewahimiza wanawake wa Wilaya ya Mbarali kuchangamkia fursa za kilimo, akisisitiza kuwa kila wilaya itafanyiwa jitihada kuhakikisha wanawake wakulima wanavuka na kunufaika zaidi. Kwa upande wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mahundi amesema kundi la wanawake wachimbaji madini litaangaliwa kwa jicho la tatu, akibainisha kuwa Wizara ya Madini haiwezi kufanya kazi peke yake bila kushirikiana na wizara yake, jambo linaloonesha umuhimu wa ushirikiano wa wizara mtambuka katika kuwainua wanawake kiuchumi.amemshukuru Mwenyekiti wa UWT Mkoa pamoja na Kamati ya Utekelezaji kwa maandalizi mazuri ya zawadi hiyo huku akiahidi wa kuendelea kushirikiana na viongozi wa wanawake mkoani Mbeya.Hata hivyo kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge, ametoa mbolea kwa wajumbe wote wa kikao hicho ambapo pia wajumbe hao wamemshukuru kwa msaada huo na kumuahidi kuutumia vizuri katika shughuli za kilimo.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment