" VIONGOZI WA DINI WAKUMBUSHWA KUONGOZWA NA DHAMIRA YA KWELI KATIKA KULINDA AMANI

VIONGOZI WA DINI WAKUMBUSHWA KUONGOZWA NA DHAMIRA YA KWELI KATIKA KULINDA AMANI



Taasisi ya Amani Tanzania (Tanzania Peace Building Initiative – TPBI) imetoa semina kwa viongozi wa Jumuiya ya Amani na Maridhiano Tanzania (JMAT) Kanda ya Ziwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujadili na kuimarisha mstakabali wa amani nchini.

Akizungumza wakati wa semina hiyo, Mwenyekiti Mtendaji wa TPBI, Askofu Amosi Joseph Muhagachi, amewakumbusha viongozi wa dini kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya tofauti za kidini, kwa kuunganisha nguvu zao katika kulinda na kuendeleza tunu ya amani kupitia umoja na mshikamano.

Askofu Muhagachi amesema viongozi wa dini ni wawakilishi wa Mungu katika jamii, hivyo wanaposhiriki katika juhudi za kutafuta na kulinda amani na utulivu wa nchi, wanapaswa kuongozwa na dhamira ya kweli na nia ya dhati ya kulisaidia Taifa bila kujikita katika misingi ya tofauti za kidini.

Ameongeza kuwa viongozi hao ni walinzi wa amani, hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kusuluhisha migogoro na kuunganisha makundi mbalimbali ya jamii, badala ya kuwa chanzo cha migogoro. Pia amesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kuwa mabalozi wa amani kwa vitendo na maneno yao ili kudumisha mshikamano wa kitaifa.

Askofu Muhagachi amewataka viongozi wa dini nchini kutambua wajibu na nafasi yao katika kulinda na kudumisha amani, kwa kutumia majukwaa yao kushauri, kukosoa na kuonyesha mwelekeo sahihi kwa jamii.

Amesema kuwa viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kuhamasisha maadili mema na mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa pale viongozi wa serikali au jamii wanapofanya makosa, wanapaswa kuonywa kwa faragha na kwa njia yenye staha ili kulinda heshima na mshikamano.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mafunzo wa Taasisi ya TPBI, Askofu Rwanga Chriss Kateti, amewakumbusha viongozi wa dini umuhimu wa kuiombea nchi ili iendelee kudumisha amani. Askofu Kateti ametaja mbinu mbalimbali zinazopaswa kutumika katika kuimarisha amani, ikiwemo utoaji wa elimu ya uraia kuanzia ngazi ya familia, shuleni, pamoja na katika nyumba za ibada kupitia mahubiri yanayohamasisha amani.

Semina hiyo imeandaliwa na taasisi ya Amani ya TPBI ( Tanzania Peace Building Initiative) ambapo washiriki wameahidi kuyatafakari mafunzo hayo na kuyafanyia kazi kwa lengo la kuendeleza maridhiano na kudumisha amani katika jamii. 

Semina hiyo inafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa St. Dominic Nyakahoja jijini Mwanza, ikianza Februari 10, 2026 na inatarajiwa kuhitimishwa Februari 11, 2026. 

Mafunzo hayo yamewakutanisha viongozi wa JMAT kutoka mikoa ya Mara, Geita, Mwanza, Kagera, Simiyu na Shinyanga, wakijadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha mshikamano, utatuzi wa migogoro pamoja na kukuza utamaduni wa amani katika jamii, huku washiriki wakisisitiza umuhimu wa kutumia nafasi zao za kiuongozi kuhamasisha maadili ya upendo, uvumilivu na mshikamano ili kudumisha amani na utulivu wa Taifa.

Mwenyekiti mtendaji TPBI adkofu Amosi Joseph Muhagachi akizungumza na washiriki wa semina.

Mkuu wa mafunzo wa Taasisi ya TPBI Askofu Rwanga Chris Kateti






 

Post a Comment

Previous Post Next Post