" WAUMINI WAHIMIZWA KUWATUNZA WATUMISHI WA MUNGU ILI KUIMARISHA HUDUMA YA INJILI

WAUMINI WAHIMIZWA KUWATUNZA WATUMISHI WA MUNGU ILI KUIMARISHA HUDUMA YA INJILI

Na Lydia Lugakila -Misalaba MediaMbeyaWaumini wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi, Usharika wa Ibala–Uyole, wamehimizwa kuendeleza moyo wa upendo, uwajibikaji na kujali kwa vitendo kwa kuwatunza watumishi wa Mungu, hatua itakayowapa nguvu na ari ya kutekeleza kazi ya Injili kwa hekima, maarifa na ufanisi mkubwa.Wito huo umetolewa na Mchungaji Greenwell Dickson Sinkwembe Mwenyekiti wa Wilaya ya Mbeya wa Kanisa la Moravian Tanzania, alipokuwa akihubiri neno la Mungu katika ibada maalum ya kumkaribisha rasmi Mchungaji Godfrey Ntinga, Mwenyekiti mpya wa Wilaya ya Uyole.Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi, Usharika wa Ibala–Uyole.Akizungumza katika ibada hiyo, Mchungaji Sinkwembe alisema Wilaya ya Mbeya inampokea Mwenyekiti wa Wilaya ya Uyole kwa shangwe na furaha kubwa, huku akiahidi kumpa ushirikiano wa dhati katika kuendeleza kazi ya Mungu ndani ya wilaya hiyo mpya.Aidha, aliwahimiza Wakristo kufanya kazi ya Mungu kwa uaminifu na bidii, ikiwemo kumtunza mtumishi wa Mungu aliyewekwa juu yao ili aweze kujikita kikamilifu katika majukumu ya kuhubiri Injili, kuwaombea waumini na kuhudumu kwa jina la Yesu Kristo bila vikwazo vya mahitaji ya msingi.Kwa upande wake, Mchungaji Edson Mwakabenga wa Kanisa la Moravian, Usharika wa Bethlehem, alilikumbusha kanisa umuhimu wa kuwatunza watumishi wa Mungu, akisisitiza kuwa Biblia ina maelekezo ya wazi kuhusu wajibu huo wa kiroho na kimaadili kwa waumini.Naye Mchungaji Godfrey Ntinga, Mwenyekiti wa Wilaya ya Uyole, aliwashukuru kwa dhati kamati ya maandalizi, wachungaji wenzake, idara zote za wilaya, dinari pamoja na mashirika kwa ukarimu, ushirikiano na sadaka walizotoa kufanikisha ibada hiyo maalum.Ameahidi kutumia kwa uaminifu nafasi aliyokabidhiwa ili kulijenga kanisa na kuwatumikia waumini kwa haki na unyenyekevu.Ameongeza kuwa ujumbe wake kwa waumini ni kutambua kuwa uaminifu ni nguzo ya baraka na mafanikio, kwani mtu anapokuwa mwaminifu kwa Mungu na katika majukumu yake, hufunguliwa milango ya neema na mafanikio ya kweli.Ikumbukwe kuwa Mchungaji Godfrey Ntinga alichaguliwa Oktoba 2025 kuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Uyole, Kanisa la Moravian Tanzania. Wilaya hiyo mpya ilizaliwa baada ya mgawanyo wa kiutawala wa Wilaya ya Mbeya, ambapo jumla ya mashirika 58 yaligawanywa na mashirika 26 kubaki chini ya Wilaya ya Uyole.Hata hivyo Mchungaji Ntinga ndiye Mwenyekiti wa kwanza kupokelewa rasmi tangu kuanzishwa kwa Wilaya hiyo ya Uyole.

Post a Comment

Previous Post Next Post