" ASKOFU AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA KUGHUSHI NYARAKA ZA ARDHI TEMEKE

ASKOFU AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA KUGHUSHI NYARAKA ZA ARDHI TEMEKE





Na Mwandishi Wetu,

Temeke, Dar es Salaam.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imemfikisha mahakamani Askofu Renatus Joseph Nyalali wa kanisa la Hosanna Assemblies of God Tanzania (HAOGT) kwa tuhuma za kughushi nyaraka za ardhi ili kujipatia kiwanja chenye thamani ya shilingi milioni 60.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Naibu Mkuu wa TAKUKURU Temeke Ismail Bukuku amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya uchunguzi uliofanywa kufuatia malalamiko kutoka kwa mmoja wa warithi na msimamizi wa mirathi ya marehemu Ally Hamad Hillal.

Uchunguzi umebaini kuwa kati ya mwaka 2021 na 2022, mtuhumiwa anadaiwa kughushi nyaraka na sahihi za wanafamilia wa marehemu kwa lengo la kujipatia umiliki wa eneo la ardhi lililopo Mtaa wa Geza Ulole, Wilaya ya Kigamboni. Eneo hilo lilinunuliwa mwaka 2008 kwa shilingi milioni 60 na kuachwa kama urithi kwa watoto wa marehemu.

Aidha, inadaiwa mtuhumiwa alitumia mwanya wa kuaminiwa na familia ya marehemu kuandaa nyaraka za uwakilishi (Power of Attorney) kwa njia isiyo halali. Nyaraka hizo zilidaiwa kutumika kupima eneo hilo na kuligawa katika viwanja tisa, ambavyo baadaye vilianza kuuzwa kwa watu mbalimbali kwa kutumia majina na sahihi za kughushi za wanafamilia.

Katika baadhi ya viwanja hivyo, uchunguzi umeonesha kuwa mtuhumiwa alijiandikisha mwenyewe kama mmiliki halali wa ardhi hiyo.

Aidha Bwn. Bukuku amesema TAKUKURU imefungua kesi ya jinai namba CC/26097/2025 katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni, huku makosa hayo yakihusishwa na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu vinavyohusu kughushi, pamoja na kifungu cha 342 kinachohusu matumizi ya nyaraka za uongo.

Taasisi hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vya rushwa, udanganyifu na uhalifu wa aina yoyote bila kujali hadhi au nafasi ya mhusika, kwa lengo la kulinda maslahi ya umma na kuhakikisha haki inatendeka.

  

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post