" DKT. MWIGULU ASISITIZA MAADILI NA UMOJA

DKT. MWIGULU ASISITIZA MAADILI NA UMOJA






_Ni katika mashindano ya kuhifadhi Qur’an wilayani Kondoa_

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema ni muhimu wa kuendeleza maadili, elimu ya dini na mshikamano wa jamii kupitia mashindano ya kuhifadhi Qur’an tukufu.

Ameyasema hayo (Jumamosi, Machi 7, 2026) wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria mashindano hayo yaliyofanyika uwanja wa Kambi ya Fisi kwenye kijiji cha Bukulu, kata ya Soera, wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.

Amesema mashindano ya aina hiyo yana mchango mkubwa katika kukuza malezi bora kwa vijana pamoja na kuimarisha misingi ya maadili mema katika jamii.

“Serikali inaunga mkono juhudi za taasisi za dini katika kuimarisha elimu ya kiroho na maadili kwa vijana. Malezi ya kidini yana nafasi muhimu katika kujenga jamii yenye amani, uvumilivu na mshikamano,” amesema Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo.

Akielezea umuhimu wa mashindano hayo, Waziri Mkuu amesema katika Qur’an sura ya pili aya ya 185, imeelezwa kuwa Qur’an imeshushwa ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. “Mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa kuisoma sana Qur’an kwa namna mbalimbali. Hongereni sana kwa kutekeleza agizo hili,” amesema.

“Nilikuwa nawaangalia usoni watoto wetu hawa, nikawa naona siyo tu kwamba wanashindana mbele yetu, niliona ni kweli wamehifadhi Qur’an. Nilishangaa kuona tunaanza na juzuu tano, zikaja 10, halafu juzuu 20 na kisha juzuu 30.”

Amewataka washiriki waendelee kuyatumia majukwaa ya mashindano ya Qur’an kuhamasisha mapenzi ya Qur’an na si ushindani peke yake. “Katika mashindano yetu haya ya leo, hakuna mshiriki ambaye amepoteza au ameshindwa, washiriki wote ni washindi kwa sababu mmejifunza, mmebeba Qur’an katika nyoyo zenu na mnaiendeleza Qur’an.”

Vilevile, Waziri Mkuu amewataka waumini wa dini hiyo watambue kuwa kuhifadhi Qur’an kichwani kunapaswa kuendane na kuiishi Qur’an kwa vitendo. “Majukwaa yote ya mashindano ya Qur’an, walimu wa Qur’an, wazazi na walezi mnawajibika kuwafundisha kwa vitendo vijana wetu kuhusu ucha-Mungu, maadili mema, uadilifu, kuhudumia na kuunganisha makundi mbalimbali katika jamii. Tusipowafundisha kuwa wachaMungu na watu wa ibada, ndivyo watakavyokuwa wakiwa watu wazima,” amesisitiza.

Mapema, Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini, Dkt. Ashatu Kijaji alisema mashindano hayo yamekuwa yakifanyika wilayani humo kwa miaka tisa mfululizo na yamelenga kuandaa kizazi ambacho kinamcha Mungu.

“Wana-Kondoa tunatamani kuona tunaandaa kizazi kilicho bora chenye kumjua Mungu. Kondoa tumeamua kuandaa Watanzania wenye hofu ya Mungu kwa kuwafundisha kitabu cha Mwenyezi Mungu na niahidi kwamba ofisi ya Mbunge haitachoka kuandaa kazi hii,” amesema.

 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post