Wakati baadhi ya watu wakitumia muda wao kwenye mitandao ya kijamii kubwabwaja na kupotosha kuwa uchumi wa Tanzania unayumba, jumuiya ya kimataifa imetoa jibu la kishindo kupitia sekta ya fedha. Tuzo tatu za kimataifa alizotunukiwa Mtendaji Mkuu wa Stanbic Tanzania, Manzi Rwegasira, jijini London nchini Uingereza, ni kielelezo tosha kuwa mfumo wetu wa kifedha uko imara na unaheshimika duniani.
Jarida la Euromoney, ambalo ni mamlaka ya juu ya tathmini ya kibenki duniani, haliwezi kuipa Benki ya Stanbic tuzo ya Benki Bora ya Kimataifa kwa mwaka wa pili mfululizo kama mazingira ya biashara na usalama wa shilingi yetu yangekuwa shakani. Hii ni tafsiri ya wazi kuwa Tanzania ina watu wenye akili na weledi wanaosimamia misingi ya fedha, na si kama inavyochorwa na "wapiga kelele" wa kidijitali.
Ushindi huu ni salamu kwa wawekezaji kuwa shilingi ya Tanzania na mfumo wake wa kibenki ni sehemu salama ya kuweka na kukuza mali. Kitendo cha Stanbic kutajwa kuwa Benki Bora ya Kimataifa kwa Wateja Maalumu (Private Banking) kinaonyesha uwezo wa kipekee wa kuunganisha uchumi wa ndani na masoko ya dunia.
Hii ina maana kuwa, licha ya changamoto za kiuchumi zinazoikumba dunia kwa sasa, Tanzania imefanikiwa kujenga "daraja la kifedha" linalowawezesha wateja kukuza mali zao nje ya mipaka kwa usalama. Heshima hii tuliyoipata jijini London inathibitisha kuwa sera zetu za kifedha zinaaminika na majopo huru ya wataalamu wa kimataifa, jambo linalowapa imani washirika wa maendeleo na wafanyabiashara wakubwa duniani.
Aidha, Tuzo ya Benki Bora kwa Kizazi Kijacho iliyonyakuliwa na Stanbic ni ujumbe mzito kwa mustakabali wa biashara za Kitanzania kuelekea Dira ya 2050. Hii inaashiria kuwa kuna maandalizi ya dhati ya kuwavusha warithi wa mali na vijana kusimamia uchumi kwa uwajibikaji.
Tunapoona taasisi zetu zikishinda tuzo za namna hii, tafsiri yake ni kwamba uchumi wetu haujajengwa kwa kubahatisha, bali kwa mikakati inayolenga uendelevu wa vizazi. Ni uthibitisho kuwa Tanzania inapiga hatua kubwa katika namna mali zinavyoundwa na kusimamiwa, ikijitofautisha na mataifa mengine yanayokumbwa na migogoro ya usimamizi wa rasilimali.
Kwa upande wa huduma kwa wateja, tuzo hiyo ya tatu inashindilia msumari kwenye ukweli kwamba mabenki yetu yameacha kufanya kazi kama ofisi za kutoa fedha tu, bali yamekuwa washauri wa kimkakati wa maamuzi ya kifedha. Huu ni ushindi wa kila Mtanzania anayeamini katika maendeleo ya nchi yake.
Hii inatupa picha kuwa Tanzania ipo sawa na mataifa mengine makubwa duniani katika kutoa huduma za kiwango cha juu. Hivyo, badala ya kusikiliza upotoshaji wa mitandaoni unaodai "Tanzania haiwezekani," tuzo hizi za Euromoney Private Banking Awards 2026 ni kioo kinachoonyesha kuwa Tanzania inawezekana na inasonga mbele kwa kasi ya ajabu katika anga za kimataifa.
Mafanikio haya ya Stanbic Tanzania ni heshima kwa nchi na ni kigezo cha tathmini kuwa uchumi wetu unaenda vyema chini ya usimamizi makini.
Tunapokuwa na benki zinazong'ara London, maana yake ni kwamba soko letu la fedha limekomaa na lina ushindani unaohitajika kuvuta mitaji mipya. Ni wakati wa Watanzania, hasa vijana, kuacha kuyumbishwa na maneno ya mitandaoni na badala yake waone fahari na fursa zilizopo katika mfumo wetu wa kifedha uliopata baraka za dunia. Tanzania inaheshimika, shilingi yetu inalindwa na weledi, na mustakabali wa mali za Watanzania upo katika mikono salama na ya kisasa.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment