Na Lydia Lugakila – Misalaba, Mbeya
Mbunge wa Jimbo la Lupa–Chunya, Masache Kasaka, ameshiriki kama mgeni maalum katika uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo uliofanyika mkoani Mbeya, ikiwa ni hatua muhimu katika kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.
Uzinduzi huo umeongozwa na mgeni rasmi, Jaji Joachim Charles Tiganga, na kufanyika katika Kijiji cha Lupatingatinga, Kata ya Lupa, wilayani Chunya. Tukio hilo limevutia wadau mbalimbali wa sekta ya sheria pamoja na viongozi wa serikali na jamii kwa ujumla.
Miongoni mwa waliohudhuria ni Jaji Gabriel Malata, majaji wengine, watumishi wa mahakama, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Alhaji Batenga. Viongozi wengine ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chunya, Kelvin Nshishi, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya, viongozi wa dini na wazee mashuhuri.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Kasaka alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuimarisha sekta ya sheria na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za haki kwa wakati.
Aidha, Kasaka aliwasisitiza wananchi kuitunza miundombinu ya mahakama hiyo pamoja na kutoa ushirikiano kwa wadau wote wa sekta ya sheria, akieleza kuwa mahakama ni sehemu muhimu ya kupata haki na kutatua migogoro katika jamii.
Kwa upande wake, mgeni rasmi alieleza kuwa serikali inaendelea kuboresha mfumo wa utoaji haki kwa kujenga na kuboresha mahakama katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na upatikanaji wa haki kwa wananchi wote.
Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa iliyonufaika na mpango huo, ambapo umejengwa mahakama za mwanzo, mahakama za watoto, mahakama zinazotembea pamoja na mahakama za wilaya. Hatua hiyo inalenga kupunguza umbali wa wananchi kusafiri kufuata huduma za kisheria na hivyo kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wote.


Post a Comment