Na Mapuli Kitina Misalaba
Viongozi na wanachama wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tawi la Tanzania (MISA TAN), ambao ni waandishi wa habari na watangazaji kutoka vyombo mbalimbali nchini, wametembelea maeneo mbalimbali ya utalii na uzalishaji mkoani Iringa ikiwa ni sehemu ya kujifunza na kutangaza fursa zilizopo mkoani humo.
Ziara hiyo imehusisha kutembelea Makumbusho ya Mkoa wa Iringa, ambapo washiriki wamepata fursa ya kujifunza historia na utamaduni wa wakazi wa mkoa huo, ikiwemo mila, desturi na historia ya machifu wa eneo hilo, hususan Mtemi Mkwawa.
Aidha, wametembelea eneo la Isimila Stone Age Site & Natural Pillars, na kujionea vivutio vya asili ikiwemo nguzo za udongo, mawe ya kale, mito na milima, pamoja na kupata maelezo ya kihistoria kuhusu eneo hilo linalotambulika kimataifa kwa urithi wake wa zama za mawe.
Katika ziara hiyo, wanachama wa MISA TAN pia wamefika Mafinga katika chuo cha mafunzo ya misitu na viwanda vya misitu, ambapo wamejifunza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji wa miche ya miti, utengenezaji wa samani pamoja na uzalishaji wa nishati mbadala ikiwemo mkaa mbadala maarufu kama kuni poa.
Vilevile, wametembelea shamba la miti la Sao Hill linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambapo wamepata elimu kuhusu usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu, ikiwa ni pamoja na juhudi za kulinda na kuendeleza sekta ya misitu nchini.
Awali akizungumzia ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema Mkoa wa Iringa una fursa za kiuchumi na vivutio vya utalii, pia una rasilimali nyingi zinazohitaji kufahamika zaidi kwa umma na wawekezaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, alisema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kauli mbiu ya kongamano hilo isemayo “Iringa Imara Itajengwa kwa Umoja na Uwajibikaji,” akieleza kuwa waandishi wa habari wana jukumu la kuandika habari zenye kujenga na kutoa suluhisho kwa changamoto za jamii.
Ziara hiyo imehitimisha shughuli za siku mbili za MISA TAN mkoani Iringa, ambapo siku ya kwanza kulifanyika kongamano la wadau wa habari lililolenga kujadili mchango wa vyombo vya habari katika maendeleo ya jamii, huku siku ya pili ikihusisha ziara ya kujifunza na kutangaza vivutio na fursa za kiuchumi zilizopo mkoani humo.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment