" WANAWAKE WATAKIWA KUZINGATIA MISINGI YA KIROHO NA KIUCHUMI ILI KUFANIKIWA

WANAWAKE WATAKIWA KUZINGATIA MISINGI YA KIROHO NA KIUCHUMI ILI KUFANIKIWA



Na Mary Sanga – Misalaba Media

Mbeya

Kufuatia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Machi 8, wanawake wameaswa kujifunza na kuzingatia mambo muhimu yatakayowasaidia kufikia mafanikio ya kiuchumi pamoja na kiroho, na kujenga familia bora.

Mafundisho hayo yametolewa na Mwalimu wa neno la Mungu, ombi Mahenge, kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma ya Hema la Maombi Mtandaoni—huduma inayohudumia zaidi ya watu elfu moja kwa masuala ya kiroho na kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwalimu Mahenge alisema wanawake wana nafasi kubwa katika kuleta mapinduzi ya maendeleo katika jamii. 

Alifafanua kwa kutumia mifano kutoka katika Biblia, akiwemo mwanamke Mshunami ambaye, kwa moyo wa ukarimu, alimshawishi mumewe kumhudumia mtumishi wa Mungu Elisha kwa chakula na malazi.

Kutokana na wema huo, baadaye walipokea muujiza wa kupata mtoto baada ya muda mrefu wa kukosa uzao.

Aidha, alimtaja pia mwanamke Abigaeli kama mfano wa busara na mchango wa wanawake katika jamii, akisisitiza umuhimu wa wanawake kuwa na hekima, moyo wa kujitoa na hofu ya Mungu.

Mwalimu Mahenge aliongeza kuwa maadhimio ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyorasimishwa mwaka 1975 kupitia mikutano ya kimataifa, yamechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha usawa wa kijinsia, hasa katika nyanja za uongozi na uwakilishi katika mabunge.

Katika mafundisho yake, aliwahimiza wanawake kujitambua, kufanya kazi kwa bidii, na kutumia maarifa ili kujikwamua kiuchumi. 

Pia alisisitiza umuhimu wa malezi bora ya familia ili kulea kizazi chenye maadili ya Kitanzania na hofu ya Mungu.

Kwa ujumla, wanawake wametakiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa kuzingatia misingi ya kiroho, kiuchumi na kijamii katika maisha yao ya kila siku.

Post a Comment

Previous Post Next Post