" MOWI CONSULTING YAWAALIKA WAFANYABIASHARA MBEYA KWENYE SEMINA YA MFUMO MPYA WA KODI (IDRAS )

MOWI CONSULTING YAWAALIKA WAFANYABIASHARA MBEYA KWENYE SEMINA YA MFUMO MPYA WA KODI (IDRAS )

 

Na Lydia Lugakila-Misalaba Media,Mbeya.

Taasisi ya kitaaluma ya uhasibu mkoani Mbeya, MoWi Consulting, imewaalika wafanyabiashara wa kada mbalimbali wakiwemo wadogo, wa kati na wakubwa, pamoja na mameneja, wamiliki wa biashara na wahasibu, kushiriki semina muhimu kuhusu mfumo mpya wa uratibu kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) unaojulikana kama IDRAS.


Semina hiyo inatarajiwa kufanyika tarehe 19 Machi 2026 katika ukumbi wa Eden, jijini Mbeya, kuanzia saa 9:00 alasiri hadi saa 12:30 jioni.


Akizungumza Machi 18, 2026 katika ofisi za MoWi zilizopo kata ya Forest, mtaa wa Magorofani, Mkurugenzi wa MoWi School of Business, Willa John Tinga, amesema kuwa semina hiyo itakuwa ya kipekee na yenye manufaa makubwa kwa wafanyabiashara, hivyo amewahimiza wote wanaolengwa kuhudhuria bila kukosa.


Tinga amesema kuwa semina hiyo itajikita katika kutoa elimu ya kina kuhusu mfumo mpya wa IDRAS ambao tayari umeanza kutumika, huku akibainisha kuwa mfumo huo umeleta mabadiliko makubwa katika uratibu wa kodi, hivyo ni muhimu wafanyabiashara kuuelewa kwa undani.


Aidha ameongeza kuwa , washiriki watapata fursa ya kujifunza namna ya kubuni na kuweka mifumo madhubuti ya ndani ya biashara zao.


"Hii itahusisha taratibu za malipo, ununuzi, ukusanyaji wa mauzo, utayarishaji wa ripoti, utoaji wa mikopo, ukusanyaji wa madeni pamoja na uendeshaji mzima wa shughuli za biashara" ameongeza Tinga


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MoWi Consulting, CPA Baraka Mori, amesema kuwa licha ya kuwepo kwa semina zilizopita, ikiwemo iliyofanyika katika ukumbi wa Beaco jijini humo, bado kuna wafanyabiashara wengi hawakupata fursa ya kushiriki au muda haukutosha kujifunza kwa kina.



Mori ameeleza kuwa tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa IDRAS Februari 9, 2026, baadhi ya wafanyabiashara wameanza kukumbana na changamoto mbalimbali, hivyo semina hii imelenga kutoa ufumbuzi wa changamoto hizo.


“Semina ya kwanza iliwakusanya watu wengi sana na muda haukutosha kugusa kila eneo pia mfumo ulikuwa bado haujaanza kutumika kikamilifu sasa umeanza kufanya kazi, hivyo tutasaidia washiriki kuelewa kwa vitendo na jinsi ya kukabiliana na changamoto zilizopo,” amesema Mori.


Ameongeza kwa Hata hivyo amewasisitiza wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi ili waweze kutumia mfumo huo mpya wa IDRAS kwa usahihi na ufanisi bila usumbufu kupitia semina hiyo.


Post a Comment

Previous Post Next Post