Na, Egidia Vedasto,
Misalaba Media, Arusha.
Jamii imekumbushwa kushirikiana katika malezi jumuishi ya watoto na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili pindi vinapotokea ili kusaidia kuvikomesha na kujenga jamii yenye upendo na maadili mema.
Akizungumza katika ziara ya kutembelea vikundi vya malezi katika shirika la SOS Children’s Villages lililopo Ngaramtoni mkoani Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Seleman Msumi, alipongeza juhudi za vikundi hivyo katika kuimarisha malezi na kupinga ukatili.
Msumi amesema kuwa katika harakati za kutokomeza ukatili ni muhimu wanaume washirikishwe kikamilifu katika malezi ya watoto.
Ameongeza kuwa baadhi ya wanaume pia hukumbwa na ukatili lakini hunyamaza, hali ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa zaidi katika jamii.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa SOS Children’s Villages mkoani Arusha, Mpeli Kalonge, amenukuu maneno ya Biblia katika kitabu cha Mithali yanayosisitiza umuhimu wa wazazi katika malezi, akieleza kuwa malezi wanayotoa yanafanana na ya kifamilia na huwasaidia watoto kutimiza ndoto zao na kuwa mfano mzuri katika jamii.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Victor Rugarabamu, amesema vikundi vya malezi vimeleta matokeo chanya kwa kusaidia watoto wengi waliokuwa hawana matumaini ya maisha.
Aidha ameongeza kuwa wizara inalenga kufikia vikundi vya malezi 200,000 ifikapo mwaka 2030 kutoka vikundi 4,060 vilivyopo sasa.
Naye mwathirika wa ukatili wa kijinsia, Mwalimu Veronica Kidemi mkazi wa Wilaya ya Arusha, aliyekatwa mkono na mume wake mwaka 2020 kutokana na wivu wa mapenzi, amesema vitendo vya ukatili mara nyingi huanza kidogo na kunyamaziwa hadi kufikia madhara makubwa.
Veronica amewataka wanawake kutoendelea kunyamaza wanapofanyiwa ukatili, bali kutoa taarifa mapema ili kuzuia matukio hayo yasigeuke kuwa vifo au ulemavu wa kudumu.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment