Na Lydia Lugakila-Misalaba, Mbeya
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limethibitisha vifo vya watu 18 vilivyotokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Machi 25, 2026 katika maeneo ya kata za Nkunga, Lupepo, Kawetele na Ikuti wilayani Rungwe.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali ilinyesha kati ya saa 6 usiku hadi saa 9:30 alfajiri, na kusababisha maporomoko ya udongo yaliyosomba nyumba zaidi ya tisa zilizokuwa zimejengwa kwa tofali mbichi.
“Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ilisababisha maporomoko ya udongo na kupelekea vifo vya watu 18, wakiwemo watu wazima wanne na watoto 14,” amesema Kuzaga.
Amebainisha kuwa miongoni mwa watu wazima waliofariki ni Chapakazi Mwasota (60), Rhoida Mwangwina (55), Gladness Chapakazi (18), Neema Mwasyema (31), Aneth Morohan (35), Obeid Shibuka (20) na Itika Manyanya (26).
Watoto waliopoteza maisha wanajumuisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari pamoja na watoto wadogo, hali inayoonyesha ukubwa wa athari za tukio hilo.
Katika tukio hilo, watu watano walijeruhiwa, wakiwemo watoto watatu wa kike na watu wazima wawili. Majeruhi hao wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Makandana iliyopo Tukuyu pamoja na Zahanati ya Chuo cha Magereza Kiwira.
“Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu huku hali zao zikifuatiliwa kwa karibu na wataalamu wa afya,” alieleza Kamanda Kuzaga.
Aidha, amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na juhudi za uokoaji katika maeneo yaliyoathirika.
“Timu za uokoaji zinaendelea na kazi katika maeneo husika huku madaktari wakifanya uchunguzi wa miili ya marehemu na kutoa huduma za awali kwa wahanga,” amesema, akiongeza kuwa Kamati ya Maafa ya Wilaya inaendelea kufanya tathmini ya tukio hilo na kuratibu utoaji wa misaada kwa waathirika.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment