*Dereva wa lori atuhumiwa kukimbia,asakwa na polisi
Na Judith Ferdinand
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limeanza msako wa dereva aliyesababisha ajali ilioua mtu mmoja na kujeruhiwi wengine wawili iliotokea mtaa wa Nyamadoke, Kata ya Nyamh’ongolo, wilaya Ilemela mkoani hapa.
Aliyefariki ni Zablon Simon, dereva bajaji huku majeruhi wakiwa ni Monica Katego,mfanyabiashara mkazi wa Buswelu na Enos Sanange, mkazi wa Nyamadoke,wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa,akizungumza katika eneo la tukio,amesema ajali ilitokea Machi 24,2026 majira ya saa 12 na dakika 30 jioni,pikipiki ya magurudumu matatu ya kubeba mizigo yenye namba za usajili MC 433 DGU, aina ya WANHOO, iliyokuwa ikiendeshwa na Zablon Simon,ilikuwa ikitokea barabara ndogo na kuingia barabara kuu,iligongana uso kwa uso na gari lenye namba T 406 EGZ, aina ya HOWO Truck, ambalo lilikuwa likitokea Buswelu kuelekea Nyamh’ongolo.
Mutafungwa amesema,baada ya kugongana uso kwa uso,dereva bajaji alipoteza maisha hapo hapo na gari hilo lilipoteza mwelekeo na kwenda kugonga banda la mgahawa lililokuwa upande wa kushoto wa barabara, ambapo walikuwepo wanawake
wawili wanaofanya biashara ya chakula katika eneo hilo na kuwasababishia majeraha.
“Wanawake hao waliokolewa wakiwa salama, kwani hawakupata majeraha makubwa, na walikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure kwa ajili ya matibabu pia mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi,”amesema Mutafungwa.
Mutafungwa amesema,chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa gari lenye namba T 406 EGZ, lililokuwa likitokea
Buswelu kuelekea Nyamh’ongolo, ambapo dereva wake alikuwa akiendesha kwa kasi katika maeneo ya makazi ya watu bila kuchukua tahadhari.
Vilevile, dereva pikipiki ya magurudumu
matatu aliingia katika barabara kuu pasipo kuchukua tahadhari.
“Juhudi za kumtafuta dereva aliyekimbia baada ya kusababisha ajali zinaendelea,atakapokamatwa, atachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,”amesema Mutafungwa.

Sanjari na hayo,alitoa wito kwa wananchi hususani madereva wa vyombo vya moto kuendelea kuzingatia matumizi sahihi ya barabara kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani pindi wanapokuwa wakiendesha vyombo vya moto.
“Kabla ya kuingia katika barabara kuu, ni lazima kujiridhisha usalama wa kulia na kushoto.Madereva walioko katika barabara kuu wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani, hasa wanapopita katika maeneo ya makazi ya watu, kwa kupunguza mwendo ili kuhakikisha usalama kwa watumiaji wengine wa barabara,”amesisitiza Mutafungwa.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment