Na Edington Mukiza Ezron, Misalaba MediaBaadhi ya wananchi wa Mtaa wa Mwinamila, Kata ya Ngokolo katika Manispaa ya Shinyanga, wameiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara ili kupunguza adha inayojitokeza mara kwa mara, hususan katika kipindi cha mvua.
Wakizungumza na Misalaba Media Machi 25, 2026, wananchi hao wamesema hali ya barabara katika eneo hilo imekuwa mbaya zaidi nyakati za masika, ambapo maji hukusanyika barabarani na mengine kuelekea kwenye makazi yao kutokana na kukosekana kwa mifumo madhubuti ya mifereji ya maji.
Mmoja wa wananchi hao, James Mwoleka, amesema changamoto hiyo imekuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu, huku akibainisha kuwa ukosefu wa mitaro ya kuelekeza maji imekuwa ni kero kubwa kwenye mtaa huo.
“Wakati wa mvua, maji yanatuingia hadi majumbani kwa sababu hayana sehemu maalum ya kupita. Tunaomba serikali itusaidie kutengeneza mitaro ili kuondoa tatizo hili na kulinda usalama wetu,” amesema Mwoleka.
Kwa upande wake, mfanyabiashara mdogo wa samaki katika soko la Ngokolo Mitumbani ambaye hakutaka kutajwa jina amesema kuwa hali hiyo inaathiri shughuli zao za kiuchumi, kwani maji ya mvua huingia katika maeneo yao ya biashara na kusababisha usumbufu mkubwa pamoja na hatari kwa afya.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwinamila, Juma Athuman Mbogo, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo, akieleza kuwa hata yeye binafsi ni miongoni mwa waathirika wa changamoto hizo hasa katika Barabara ya Mwandu (Mwandu Road).
Amesema suluhisho la kudumu ni ujenzi wa mitaro ya kisasa ili kuelekeza maji hayo, kwani kwa sasa maji hayo hukosa mwelekeo na kusababisha uharibifu wa barabara pamoja na makazi ya wananchi.
Mbogo amebainisha baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi kuwa ni Barabara ya Mwandu, barabara ya Sokoni Mitumbani pamoja na Barabara ya Mama Tatu. Ameongeza kuwa tayari wameshawafikishia viongozi wa eneo hilo akiwemo diwani wa Kata ya Ngokolo pamoja na mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini ikiwa lengo ni kutafuta suluhisho la kudumu.
Hata hivyo Mbogo, amewaomba wananchi kuwa na subira wakati juhudi za kutatua changamoto hiyo zikiendelea, akisisitiza kuwa viongozi wao wanatambua tatizo hilo na wanalifanyia kazi kwa kushirikiana ili kupunguza madhara kwa wakazi wa eneo hilo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwinamila, Juma Athuman Mbogo, akizungumza na Misalaba Media
Baadhi ya maeneo ya barabara korofi katika mtaa wa Mwinamila.SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment