Na Mapuli Kitina Misalaba
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kuokoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya
Shilingi 51,752,600 kufuatia ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa
miradi ya maendeleo katika Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa kwa vyombo vya
habari, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, amesema hatua hiyo
imechukuliwa baada ya kubainika kuwa mzabuni wa mradi wa ujenzi wa nyumba ya
mtumishi katika Shule ya Msingi Magongwa, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala,
alinunua vifaa vya ujenzi lakini hakuvifikisha kwenye eneo la mradi.
Vifaa vilivyookolewa ni pamoja na nondo, vigae
(25x40), vifaa vya umeme, vifaa vya maji, vyoo, gypsum board na rangi. Kufuatia
ufuatiliaji huo, TAKUKURU ilimtaka mzabuni kuwasilisha mara moja vifaa hivyo
katika mradi husika ili kuhakikisha thamani ya fedha za umma inalindwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kipindi cha Oktoba
hadi Desemba 2025, TAKUKURU imefuatilia jumla ya miradi 18 ya maendeleo yenye
thamani ya Shilingi 3,536,123,370 katika Mkoa wa Shinyanga.
Ufuatiliaji huo umeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa
kuimarisha uwajibikaji, kuzuia ubadhirifu wa fedha za umma na kuhakikisha
miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa viwango vinavyokusudiwa kwa manufaa ya
wananchi.
TAKUKURU imewataka watendaji wa umma na wazabuni
kuzingatia mikataba na taratibu za ununuzi ili kuepusha hatua za kisheria, huku
wananchi wakihimizwa kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa au
ubadhirifu kupitia namba 113 bure.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment