Na Mwandishi wetu, Misalaba MediaJimbo la Tunduru Kusini linaelekea kuandika historia mpya ya maendeleo kufuatia mkakati wa kujenga barabara za kiwango cha lami katika baadhi ya maeneo muhimu, hatua inayotarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi na kurahisisha usafiri pamoja na usafirishaji wa mazao kwa mwaka mzima.Hatua hiyo imekuja baada ya ziara ya tathmini iliyofanywa na Mbunge wa Jimbo hilo, Mhandisi Fadhili Chilombe, kwa kushirikiana na Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Silvester Chinengo, waliokagua hali ya miundombinu na kuweka mikakati ya maboresho ya muda mfupi na mrefu.Kwa mujibu wa viongozi hao, pamoja na matengenezo ya kawaida yatakayofanyika katika baadhi ya barabara, yapo maeneo yatakayopandishwa hadhi na kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuyawezesha kufunguka zaidi kiuchumi na kijamii.Kwa miaka mingi, changamoto ya miundombinu imekuwa kikwazo kikubwa katika jimbo hilo, hasa kipindi cha mvua ambapo barabara nyingi huharibika, magari hukwama na mazao ya wakulima kushindwa kufika sokoni kwa wakati. Hali hiyo imekuwa ikiathiri biashara ndogo na za kati pamoja na upatikanaji wa huduma za kijamii.Tunduru Kusini, ambayo uchumi wake unategemea zaidi kilimo, inatarajiwa kunufaika kwa kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza thamani ya mazao na kuvutia uwekezaji katika maeneo ya miji na vijiji vikubwa vitakavyopata lami.Wakazi wa jimbo hilo wameeleza matumaini yao kuwa ujenzi wa barabara hizo utarahisisha upatikanaji wa huduma za afya na elimu, kufungua fursa za ajira kwa vijana na wanawake na kubadilisha taswira ya maendeleo ya eneo hilo.Iwapo mpango huo utatekelezwa kama ulivyopangwa, Tunduru Kusini itaingia katika hatua mpya ya maendeleo, ikihama kutoka changamoto za vumbi na matope kuelekea miundombinu imara inayoweza kuhudumia wananchi kwa majira yote ya mwaka.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254




Post a Comment