" WANAWAKE TUGHE SHINYANGA WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA MATENDO YA HURUMA

WANAWAKE TUGHE SHINYANGA WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA MATENDO YA HURUMA

 


Na Mapuli Kitina Misalaba

Wanawake wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Mkoa wa Shinyanga wameshiriki kikamilifu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Ushetu, Wilaya ya Kahama, huku wakitumia fursa hiyo kuonyesha mchango wao katika maendeleo ya jamii.

Wanawake hao walipata nafasi ya kuzungumza wakati Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, alipokuwa akitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali yaliyokuwa yakitoa elimu na kuonesha shughuli zao katika eneo la maadhimisho hayo.

Akizungumza katika banda la TUGHE, Mwenyekiti wa Kamati za Wanawake wa TUGHE Mkoa wa Shinyanga, Experantia Misalaba, amesema wanawake wa kamati hiyo wanaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwapa kipaumbele wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

“Wanawake wa Kamati za TUGHE Mkoa wa Shinyanga tunaunga mkono juhudi za Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupa kipaumbele sisi wanawake,” amesema Misalaba.

Ameeleza kuwa wanawake wa TUGHE hushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo ikiwemo kutoa mafunzo, warsha na makongamano yanayolenga kuwawezesha wanawake na watumishi katika sekta ya serikali na afya.

Aidha, amesema kamati ya wanawake ya TUGHE mkoa huo imekuwa na utaratibu wa kufanya matendo ya huruma kila mwaka ifikapo Machi 8, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa vitendo.

Amesema mwaka huu wanatarajia kutoa msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Iselamagazi (Nhindo) vikiwemo machela ya kusafirisha wagonjwa, thermometers (vipima joto), mizani ya kupimia uzito, stethoscope, mashine za kupimia shinikizo la damu (BP machine) pamoja na mashine za kupimia sukari kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza baada ya kusikiliza maelezo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewapongeza wanawake wa TUGHE kwa moyo wao wa kujitolea kusaidia jamii.

“Hongereni sana kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali katika jamii kwa kufanya matendo ya huruma. Hii inaonyesha namna wanawake wanavyoshiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii,” amesema Mhita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, ameishukuru Kamati ya Wanawake wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Mkoa wa Shinyanga kwa msaada wa vifaa tiba walivyotoa katika Hospitali ya Iselamagazi, akisema hatua hiyo ni mchango muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi. 

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kimkoa yamefanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi Kufikia Dira ya 2050.”

Mwenyekiti wa Kamati za Wanawake wa TUGHE Mkoa wa Shinyanga, Experantia Misalaba, akizungumza.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akitoa pongezi zake.Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, akiishukuru Kamati za Wanawake wa TUGHE Mkoa wa Shinyanga.



 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post