" ELIMU YA MAADILI NA UKATILI WA KIJINSIA YATOLEWA NA SMAUJATA SHINYANGA

ELIMU YA MAADILI NA UKATILI WA KIJINSIA YATOLEWA NA SMAUJATA SHINYANGA

Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) imetoa elimu ya maadili na kupinga ukatili wa kijinsia kwa vijana wa kiume katika Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Wanaume.

Elimu hiyo ilitolewa Aprili 24, 2026 kwa wanafunzi wavulana wa Shule ya Sekondari Old Shinyanga, ambapo lengo kuu lilikuwa kuwaandaa vijana hao kuwa walezi bora wa jamii na taifa la kesho pamoja na kuwahamasisha kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Mwarabu Akimu Mwimbili, alisema vijana wa kiume wanapaswa kuzingatia maadili ya Kitanzania na kujiepusha na vitendo vinavyokiuka maadili hayo. Alisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa katika mamlaka husika pale vitendo vya ukatili au ukiukwaji wa maadili vinapobainika.

Kwa upande wake, Katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Daniel Sibu, aliwataka vijana kuepuka tamaa na starehe za muda mfupi ambazo zinaweza kuharibu maisha yao, akitaja baadhi ya vitendo hivyo kuwa ni pamoja na michezo ya kubashiri na matumizi mabaya ya muda katika maeneo ya starehe.

Aidha, viongozi hao waliwaasa vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na matumizi holela ya simu, wakieleza kuwa mambo hayo yanaweza kuathiri ndoto na mustakabali wao.

Naye Kiongozi wa Idara ya Utamaduni, Makongamano na Utalii Kitaifa, Daniel Kapaya, alisisitiza umuhimu wa vijana kuendeleza utamaduni wa Kitanzania na kuwa na uthubutu, akieleza kuwa wao ni wazazi wa baadaye na walinzi wa maadili katika jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi walitoa wito kwa viongozi na jamii kwa ujumla kuchukua hatua dhidi ya mienendo ya baadhi ya wasanii wanaokiuka maadili ya Kitanzania, wakieleza kuwa tabia hizo huigwa na vijana na kuchangia kuporomoka kwa maadili.

Hata hivyo, vijana hao walihimizwa kukataa ukatili wa kijinsia katika aina zote na kuachana na mfumo dume, wakielezwa kuwa hata baadhi ya wanaume huathirika na vitendo vya ukatili kutokana na mfumo huo.

 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post