Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa
Jamii Tanzania (SMAUJATA) Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, mkoani
Shinyanga, Bi. Nives Nyoni, ameongoza juhudi za uokoaji wa mtoto wa kike mwenye
umri wa miaka 10 aliyedaiwa kukumbwa na vitendo vya ukatili kutoka kwa mama
yake mzazi.
Tukio hilo lilitokea Aprili 23, 2026 majira ya saa
mbili usiku katika kijiji cha Isaka Station, ambapo mtoto huyo alikimbilia
nyumbani kwa Bi. Nyoni kuomba msaada, akieleza kuwa amekuwa akipigwa mara kwa
mara, kunyimwa haki ya masomo pamoja na kufanyiwa vitendo vya mateso.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Bi. Nyoni alimpatia
hifadhi ya muda mtoto huyo nyumbani kwake na kuwashirikisha viongozi wengine wa
SMAUJATA akiwemo Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bi. Nabila Kisendi
ambapo Asubuhi iliyofuata, kwa kushirikiana na mtoto huyo, walimpeleka katika
kituo cha polisi kwa ajili ya hatua zaidi dhidi ya mzazi anayetuhumiwa.
Katika kufanikisha zoezi hilo, SMAUJATA ilishirikiana
na maafisa ustawi wa jamii wa Halmashauri ya Msalala akiwemo Afisa Richard
Ng’ondya, Ignace Lufulila pamoja na Bi. Magori, watendaji wa eneo husika na
mkuu wa kituo cha polisi, ambapo kwa pamoja walitafuta suluhisho la kudumu kwa
mtoto huyo.
Baada ya tathmini, ilibainika kuwa mama mzazi wa mtoto
huyo ana changamoto ya afya ya akili, hali iliyochangia kuchukuliwa kwa uamuzi
wa kumkabidhi mtoto kwa baba yake mzazi anayeishi Misungwi, mkoani Mwanza.
Mwenyekiti wa SMAUJATA, Nabila Kisendi, pamoja na
Mwenyekiti wa Kata, Bi. Sophia Emanuel, walisisitiza umuhimu wa mzazi huyo wa
kiume kuhakikisha anampatia mtoto malezi bora, huku wakiahidi kuwa taasisi hiyo
itaendelea kufuatilia ustawi wa mtoto huyo hata baada ya kuhamishiwa kwa baba
yake.
Imeelezwa kuwa mtoto huyo, alionyesha hitaji kubwa la
kuishi na baba yake tofauti na ilivyo kwa watoto wengi wanaopendelea malezi ya
mama, hali iliyotafsiriwa kuwa ni matokeo ya mazingira magumu aliyokuwa
akipitia.
Kwa mujibu wa taarifa, mtoto huyo alikumbwa na ukatili
uliodaiwa kujumuisha kupigwa, kubamizwa ukutani na kufanyiwa vitendo vingine
vya mateso, hali iliyomlazimu kutafuta msaada.
SMAUJATA imewapongeza maafisa na wadau wote walioshiriki katika zoezi hilo kwa ushirikiano wao, huku wakisisitiza kuendelea kupinga ukatili dhidi ya watoto na kuhakikisha haki zao zinalindwa.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment