Na Lydia Lugakila – Misalaba Media
Mbeya
Mhadhiri msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya (CUoM), Saruni Kisambu, amewaasa wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Airport iliyopo Iyela, Mwanjelwa mkoani Mbeya, kuhakikisha wanalipa ada za shule kwa wakati ili kuwaondolea wanafunzi msongo wa mawazo unaoweza kuwaathiri kisaikolojia na kudhoofisha maendeleo yao ya kitaaluma.
Akizungumza akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya 10 ya kidato cha sita ya shule hiyo yaliyofanyika April 24,2026, Kisambu alisema ucheleweshaji wa ada unawaweka wanafunzi katika hali ngumu ya kisaikolojia, hali inayoweza kuwafanya washindwe kuzingatia masomo yao ipasavyo.
Kauli ya mgeni rasmi ilifuata risala ya shule iliyosomwa na Mkuu wa Shule, Ayubu Malambugi, iliyobainisha changamoto ya baadhi ya wazazi na walezi kutolipa ada kwa wakati, jambo linaloathiri uendeshaji wa shule na maendeleo ya wanafunzi.
Katika kuunga mkono juhudi za maendeleo ya shule hiyo, Kisambu alichangia kiasi cha shilingi laki mbili na nusu.
Akifafanua zaidi, Kisambu alisema mwanafunzi anapofahamu kuwa ada haijalipwa, hupoteza uhuru na kujiamini hata anapokuwa karibu na walimu, hali inayomfanya ashindwe kushiriki kikamilifu katika masomo.
“Mwanafunzi akijua mzazi wake hajalipa ada, anakuwa hana uhuru hata anapomuona mwalimu, jambo linalomfanya ashindwe kusoma vizuri,” alisema.
Aliongeza kuwa wakati mwingine wanafunzi hulazimika kurudi nyumbani kuwakumbusha wazazi kuhusu ada, hali inayosababisha kupoteza muda wa masomo darasani na kudidimiza taaluma yao.
Aliwahimiza wazazi na walezi kuwajibika ipasavyo na kutumia fursa ya malipo ya ada kwa awamu yanayotolewa na shule binafsi, huku akisisitiza umuhimu wa uaminifu katika utekelezaji wa makubaliano hayo.
Mahafali hayo yamefanyika kwa mafanikio makubwa na kuvutia wadau mbalimbali wa elimu mkoani Mbeya.
Ikumbukwe kuwa Shule ya Sekondari Airport inamilikiwa na shirika binafsi la ISRANI chini ya Mkurugenzi wake Nikuswiga Malambugi ambapo Ilianzishwa mwaka 2007 na inatoa elimu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, ikiwa na michepuo ya HGL, HKL na HGE, pamoja na huduma za kutwa na bweni.
Katika hatua nyingine risala yake, Mkuu wa Shule hiyo Ayubu Malambugi ilieleza namna ucheleweshaji wa ada unavyokwamisha maendeleo ya shule, hususan katika uboreshaji wa miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo vitabu na kuwa hali hiyo husababisha wanafunzi kupoteza vipindi wanapofuatilia masuala ya ada.
Mkuu huyo wa shule alitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kushirikiana na shule katika kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kitaaluma na kinidhamu, hali inayochangia kushuka kwa kiwango cha taaluma na maadili.
Vilevile, ameongeza kuwa baadhi yao hushindwa kuwaleta wanafunzi wa madarasa ya mitihani kuishi bweni kama inavyotakiwa.
Hata hivyo, alisema shule imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha taaluma, ikiwemo kuhakikisha walimu wanamaliza mitaala kwa wakati, kufanya mazoezi ya mitihani mara kwa mara na kutoa masahihisho, wanafunzi wa madarasa ya mitihani kukaa bweni, pamoja na kushirikiana na shule nyingine katika mitihani ya kujipima.
Pia, shule hutoa motisha kwa wanafunzi na walimu wanaofanya vizuri, na kusaidia wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Shule, katika matokeo ya kidato cha sita kwa miaka minne iliyopita (2022–2025), hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la nne wala sifuri tangu kuanzishwa kwa masomo ya A-Level shuleni hapo, jambo linaloonyesha mafanikio ya kitaaluma ya shule hiyo.
Kwa upande wake, Kisambu ambaye amekuwa mgeni rasmi wa mahafali hayo aliwataka wahitimu kuendelea kuzingatia maadili mema waliyojifunza, kujitambua na kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa ili kufikia malengo yao ya maisha.
Naye Mkurugenzi wa shule hiyo, Nikuswiga Malambugi, alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, imekuwa na mchango mkubwa kwa jamii kwa kutoa ajira na kusaidia vijana kupata elimu bora huku akieleza kuwa baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu wamepata ajira kupitia taasisi hiyo.
Malambugi,aliongeza kuwa shule ya Sekondari Airport ina jumla ya walimu 20 na wafanyakazi wasio walimu 10, huku shule za awali na msingi za Kiingereza za Malambugi zikiwa na watumishi 12, hivyo kufikisha jumla ya ajira 42 zinazotolewa na taasisi hiyo.
Aidha, Mkurugenzi huyo aliwapongeza wahitimu 35 wa kidato cha sita mwaka 2026 na kuwashukuru wazazi kwa kuiamini sekta binafsi ya elimu.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo aliwasisitiza wahitimu hao kuendelea kuwa na nidhamu na maadili mema ili kufanikisha ndoto zao za maisha.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254





Post a Comment