Na Lydia Lugakila-Misalaba media
Mbeya
Kutokana na matokeo ya kidato cha nne na kidato cha sita kuonyesha ufaulu wa hali ya juu mwaka 2025 katika Shule ya Sekondari Sebama, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya, Saruni Kisambu, ametoa pongezi kwa wakurugenzi wa shule huria ya Sebama kwa kuongoza kitaifa mara mbili mfululizo.
Mhadhiri Kisambu alitoa pongezi hizo akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha sita yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mkapa uliopo jijini Mbeya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kisambu alielezea umuhimu wa elimu na tumaini lililopo ndani yake, akisema kuwa ameijifunza Sebama kama “tumaini la wanyonge” — yaani wale waliokuwa wakielekea kukata tamaa baada ya kufeli, lakini wanapopata fursa ya kusoma Sebama hurudi tena kwenye matumaini na hatimaye kurejea katika mwelekeo sahihi wa maisha yao ya kielimu.
Alifafanua kuwa mara nyingi mwanafunzi anayefeli kidato cha nne au cha sita anaweza kurejea Sebama, kusoma upya, na hatimaye kujiunga na chuo kikuu, akikutana tena na wale waliopata daraja la juu tangu awali tofauti ikiwa ni miaka michache tu.
Aidha, Kisambu alisema wamekuwa wakishuhudia wanafunzi wengi waliotoka Sebama wakifanya vizuri katika vyuo vikuu, ikiwemo katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya (CUoM), jambo linalothibitisha ubora wa elimu inayotolewa na shule hiyo.
“Hii imetufundisha kwamba mwanafunzi akipata hata daraja la mwisho, hatupaswi kumhukumu kuwa hana uwezo kwani bado kuna nafasi nyingine ya kumsaidia kufikia ndoto zake,” alisisitiza Kisambu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Nyota James, akizungumza kwa niaba ya Mwakilima, alieleza mbinu zinazotumika kufanikisha ufaulu huo na kuwa hutumia mfumo wa kujituma kwa kiwango cha juu, ambapo masomo yanayopaswa kufundishwa kwa muda mrefu hufundishwa kwa muda mfupi kwa ufanisi mkubwa.
Alibainisha kuwa masomo ya miaka miwili hufundishwa kwa mwaka mmoja, ya miaka minne kwa miaka miwili, na yale ya miaka sita kwa miaka mitatu, ili kumuwezesha mwanafunzi kufikia ndoto zake kwa haraka na kuendelea na hatua inayofuata ya elimu.
Nyota aliongeza kuwa uwepo wa walimu bora wanaojituma usiku na mchana ni moja ya sababu kuu ya mafanikio ya shule hiyo.
Alisema vijana wengi hukwama katika shule nyingine, lakini wanapofika Sebama ndoto zao za kielimu hufufuka, kwani wamekuwa wakifaulu kwa kiwango kikubwa.
Wanafunzi wa mfumo wa QT huweza kupanda kutoka kidato cha pili kwenda kidato cha tatu, na kutoka kidato Cha nne kwenda kidato cha tano kwa mafanikio makubwa, na hatimaye kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali kwa idadi kubwa kila mwaka.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025, kidato cha pili (QT) waliiongoza kitaifa kwenye mfumo wa open school kwa ufaulu wa zaidi ya asilimia 98.
Katika kidato cha nne, wanafunzi 357 walifaulu na kujiunga na kidato cha tano, huku kidato cha sita pia kikiongoza kitaifa mwaka huo.
Uongozi wa shule hiyo ulitoa shukrani kwa Mungu kwa namna anavyowawezesha kufikia mafanikio hayo makubwa.
Katika hatua nyingine, Salome Sengo, Afisa Masoko kutoka Chuo Kikuu cha Jordan kilichopo mkoani Morogoro, kwa niaba ya chuo hicho, alikabidhi vifaa vya michezo kwa wanafunzi wa Sebama, ikiwa ni pamoja na jozi mbili za jezi za mpira wa miguu na mpira wa mikono.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment