Na John Bukuku, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo katika Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Dkt. Yona Mwalwisi, ameonya kuwa matumizi holela ya dawa, hususan antibiotiki, yanaendelea kuwa chanzo kikuu cha ongezeko la usugu wa dawa nchini, hali inayotishia mafanikio ya matibabu na afya ya umma kwa ujumla.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Fullshangwe Blog, jijini Dar es Salaam, Dkt. Mwalwisi, amesema kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali na taasisi mbalimbali za afya, bado kuna changamoto kubwa ya wananchi kujitibu wenyewe bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, huku akisisitiza kuwa tabia hiyo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kuibuka na kuenea kwa vimelea vinavyoshindwa kutibika kwa dawa zilizopo. Akisema kuwa
“Matumizi yasiyo sahihi ya dawa, ikiwa ni pamoja na kutozingatia dozi, kutumia dawa bila vipimo, au kutumia dawa zisizo na ubora, yanachangia vimelea kujenga usugu dhidi ya antibiotiki,” amesema.
Aidha, Ameeleza kuwa dawa zimegawanywa katika makundi kulingana na matumizi yake, ambapo baadhi zinapaswa kutolewa kwa cheti cha daktari pekee, huku nyingine zikiruhusiwa kupatikana kwa urahisi. Hata hivyo, amebainisha kuwa bado kuna baadhi ya watoa huduma wanaokiuka taratibu kwa kutoa dawa zinazohitaji usimamizi maalum bila kufuata sheria, jambo linalochochea matumizi mabaya ya antibiotiki.
Pia, Dkt. Mwalwisi, amebainisha kuwa TMDA kwa kushirikiana na Baraza la Famasi imekuwa ikiendesha ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya dawa ili kuhakikisha sheria, kanuni na maadili vinafuatwa. Aidha taasisi hizo zimekuwa zikitoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya dawa ili kupunguza hatari ya usugu wa dawa.
Ameongeza kuwa kuna mifumo madhubuti ya ufuatiliaji wa dawa kuanzia hatua ya uagizaji, usambazaji hadi uuzaji wa rejareja, hususan kwa dawa zinazohitaji cheti cha Daktari. Aidha, ameeleza kuwa dawa zenye asili ya kulevya husimamiwa kwa umakini wa hali ya juu, zikiagizwa kupitia Bohari ya Dawa na kuhifadhiwa kwa kufuata taratibu maalum za usalama.
Katika kuhakikisha ubora wa Dawa, Dkt. Mwalwisi ameeleza kuwa TMDA inafanya kazi ya kudhibiti na kukagua dawa zote zinazoingizwa nchini na zinazozalishwa ndani ya nchi ili kuhakikisha zinakuwa salama, bora na zenye ufanisi. Hatua hii inalenga kuzuia uwepo wa dawa zisizokidhi viwango ambazo zinaweza kuchangia kuongezeka kwa usugu wa dawa.

Wakati mamlaka zikiongeza juhudi za udhibiti, wataalamu wa afya wanaendelea kuonya juu ya kasi ya kuongezeka kwa usugu wa antibiotiki. Pia amesema kuwa tatizo hilo linaongezeka kutokana na uwepo wa vimelea sugu vinavyoonesha uwezo mkubwa wa kustahimili dawa nyingi kwa wakati mmoja (multidrug resistance).
Aidha, Dkt. Mwalwisi, amevitaja vimelea vinavyoongoza katika usugu huo kuwa ni pamoja na Staphylococcus aureus (MRSA), Escherichia coli, na Klebsiella pneumoniae vinavyozalisha ESBL, pamoja na bakteria kama Pseudomonas aeruginosa na Acinetobacter baumannii, amebainisha kuwa Vimelea hivo vina uwezo mkubwa wa kuhimili antibiotiki mbalimbali, hali inayofanya matibabu kuwa magumu zaidi na kuongeza hatari kwa wagonjwa.
Ameongeza kuwa umuhimu wa vipimo vya maabara katika kudhibiti usugu wa dawa ni mkubwa, akitaja vipimo kama Culture and Sensitivity, Kirby-Bauer Disc Diffusion na teknolojia ya kisasa ya PCR kuwa vinasaidia kubaini aina ya vimelea na dawa inayoweza kufanya kazi dhidi yake.
Hata hivyo, ameeleza kuwa sekta ya maabara bado inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo upungufu wa vifaa, vitendanishi na wataalamu, hali inayoweza kuathiri ubora wa matokeo na kuchangia matumizi yasiyo sahihi ya dawa.
Dkt. Mwalwisi ametoa wito kwa wananchi kuepuka kujitibu wenyewe na badala yake kufika katika vituo vya afya kupata vipimo na ushauri wa kitaalamu kabla ya kutumia dawa. Pia amesisitiza umuhimu wa kununua dawa katika maeneo yanayotambulika kisheria ili kulinda afya zao.

Kwa upande wake, Prof. Mtebe Venance Majigo kutoka Idara ya Microbiolojia na Immunology ambaye pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), , amesema kuwa tafiti zinaonesha ongezeko la usugu wa antibiotiki nchini, hasa kwa bakteria wanaosababisha maambukizi ya njia ya mkojo, vidonda na damu.
Prof. Majigo amesema kuwa wagonjwa wanaopata maambukizi wakiwa hospitalini wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata vimelea sugu kuliko wale wanaopata maambukizi nje ya hospitali. Akisema kuwa
“Maambukizi ya hospitalini mara nyingi huhusisha bakteria wenye usugu mkubwa zaidi wa antibiotiki, jambo linalofanya matibabu kuwa changamoto kubwa,” amesema Prof. Majigo
Pia, Ameongeza kuwa mbinu kuu ya kufuatilia usugu wa dawa ni kupitia vipimo vya maabara vinavyobaini uwezo wa dawa kuua bakteria, huku matumizi ya teknolojia ya genomic surveillance yakiwa bado katika hatua za awali nchini.
Aidha, Prof. Majigo, ameeleza kuwa takwimu za miaka mitano hadi kumi iliyopita zinaonesha kuongezeka kwa usugu hata kwa dawa ambazo hapo awali zilikuwa hazitumiki sana, hali inayochangiwa na matumizi yasiyo sahihi ya antibiotiki kwa binadamu na mifugo pamoja na usambaaji wa vimelea sugu katika mazingira ya huduma za afya.

Kwa Mujibu Takwimu na Tafiti kutoka majukwa ya Tafiti mbalimbali na TMDA pia zinaonesha kuwa Tanzania ina matumizi makubwa ya antibiotiki, hususan aina ya amoxicillin, metronidazole na tetracycline. Zaidi ya asilimia 90 ya matumizi hayo yako katika kundi la dawa zinazopaswa kupatikana kwa urahisi, jambo linaloibua wasiwasi juu ya uwezekano wa matumizi yasiyodhibitiwa.
Wataalamu wanaonya kuwa usugu wa dawa una madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza muda wa kulazwa hospitalini, kuongeza gharama za matibabu na kuongeza vifo vinavyoweza kuzuilika. Aidha, hali hiyo inaathiri pia mafanikio ya huduma nyingine za afya kama upasuaji na matibabu ya magonjwa sugu.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, wataalamu wanashauri kuimarishwa kwa mifumo ya matumizi sahihi ya dawa (antimicrobial stewardship), kuboresha huduma za maabara, kudhibiti maambukizi hospitalini na kuongeza elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya antibiotiki.
Kwa ujumla, usugu wa dawa unaendelea kuwa tishio kubwa linalohitaji hatua za haraka na za pamoja kutoka kwa wadau wote wa sekta ya afya. Bila kudhibiti matumizi ya dawa na kuimarisha mifumo ya afya, hatari ya kupoteza ufanisi wa antibiotiki itaendelea kuongezeka, na hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi wengi.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment