Mwanasiasa , Odero Charles Odero, ametoa ushauri kwa Serikali kutunga sheria mahususi itakayosimamia mchakato wa maridhiano ya kitaifa ili kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi thabiti wa mazungumzo na utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa.
Akizungumza katika mahojiano na moja ya televisheni za mtandaoni kuhusu mustakabali wa nchi baada ya kukabidhiwa kwa ripoti ya Tume ya Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, Odero amesema anaikubali ripoti hiyo na kuongeza kuwa maridhiano ya kweli hayawezi kupatikana kwa mazungumzo ya hiyari pekee, bali yanahitaji mfumo wa kisheria utakaotoa muongozo kama ilivyokuwa katika mchakato wa utafutaji wa Katiba, akisisitiza kuwa "maridhiano yanapaswa kuanza na sheria."
Odero ameeleza kuwa wakati umefika kwa Watanzania kukaa katika makundi mbalimbali ili kuitafakari na kuijadili ripoti hiyo kwa kina, kwa lengo la kutafuta namna bora ya kusonga mbele kama taifa moja.
Amesisitiza kuwa katika majadiliano hayo, ni jambo la msingi kwa wananchi na viongozi kutumia lugha ya staha, upendo, na inayojenga badala ya kutumia lugha za chuki au uchochezi zinazoweza kuligawa taifa.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, lugha njema ndiyo msingi wa kuijenga Tanzania mpya yenye kuvumiliana, huku akionya kuwa upinzani usio na tija hautasaidia nchi kujikwamua kutoka katika changamoto ilizopitia.
Aidha, Odero ametoa rai kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa fidia au faraja kwa familia zilizopoteza wapendwa wao kama sehemu ya kuponya makovu na kurejesha matumaini kwa waathirika wa matukio yaliyochunguzwa.
Amekiri kuwa ingawa ripoti ya tume haiwezi kujitosheleza kwa asilimia mia moja, inapaswa kutazamwa kama "mti unaoota na kukua" ambao unahitaji maboresho ya mara kwa mara. Amewataka Watanzania kuangalia udhaifu uliojitokeza kama fursa ya kufanya marekebisho na kuunga mkono juhudi za maridhiano zinazopigania mshikamano wa taifa na amani ya kudumu.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment