" Watano mbaroni tuhuma za wizi wa Sh.milioni 40 Tabora

Watano mbaroni tuhuma za wizi wa Sh.milioni 40 Tabora






Wananchi wa Mkoa wa Tabora wametakiwa kuwa makini na matapeli wanaojifanya mawakala wa huduma za kifedha, kufuatia kukamatwa kwa watu watano wanaotuhumiwa kuhusika na wizi wa shilingi milioni 40 kutoka kwa mfanyabiashara wa Wilaya ya Kaliua.

Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linawashikilia watuhumiwa hao, waliokamatwa katika nyakati tofauti wakiwa wanaendelea na shughuli zao za kawaida ndani ya mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 28, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amesema watuhumiwa wawili kati yao, Marseli Gwasima na Fred Ricardo, walijifanya wahudumu wa kampuni ya mawasiliano na kumtapeli mfanyabiashara, Fatuma Nasoro.

Amesema mfanyabiashara huyo wa khanga na vitenge alitapeliwa fedha hizo baada ya watuhumiwa kumshawishi na hatimaye kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti yake ya benki kwenda kwenye namba zao za simu.

“Kimsingi walijitambulisha kama wahudumu wanaosajili huduma za Lipa Namba kwa wafanyabiashara. Tunatoa onyo kali kwa matapeli wote kuwa hatutavumilia vitendo vya kihalifu mkoani Tabora,” amesema.

Ameongeza kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ipo macho kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaimarishwa wakati wote.

Aidha, amewataka wananchi kuwa waangalifu wanapopokea huduma kutoka kwa watu wanaojitambulisha kama mawakala au watoa huduma wa kampuni za mawasiliano, na kuhakikisha wanathibitisha uhalali wao.

Kwa upande wake, mhanga wa tukio hilo, Fatuma Nasoro, ameishukuru Serikali kwa juhudi za kuwakamata watuhumiwa hao na kuomba sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine wanaojihusisha na vitendo vya utapeli.

Post a Comment

Previous Post Next Post