" WATANZANIA 27 WANUFAIKA NA TUZO YA MWALIMU NYERERE TANGU KUANZISHWA KWAKE

WATANZANIA 27 WANUFAIKA NA TUZO YA MWALIMU NYERERE TANGU KUANZISHWA KWAKE

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 8, 2026 jijini Dodoma,wakati akitangaza rasmi kufanyika kwa hafla ya nne ya utoaji wa tuzo ya Taifa ya Mwalimu Julius Nyerere ya Uandishi Bunifu 2026.

Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2026,Prof. Penina Mlama,akielezea jinsi washiriki wa tuzo hizo walivyoshiriki kwa wingi.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametangaza rasmi kufanyika kwa hafla ya nne ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2026, akisisitiza kuwa tuzo hizo zimeendelea kuwa chachu muhimu ya kukuza fasihi ya Kiswahili na kuibua vipaji vya waandishi bunifu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 8, 2026 jijini Dodoma, Prof. Mkenda amesema hafla hiyo itafanyika Aprili 13, 2026 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Super Dome, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, aliyetoa mchango mkubwa katika kukuza lugha ya Kiswahili na uandishi wa fasihi.

Waziri Mkenda,ameeleza kuwa tuzo hizo zimeendelea kuvutia washiriki wengi zaidi kila mwaka kutoka ndani na nje ya nchi.

"Kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), ambayo inaratibu tuzo hizo kwa kushirikiana na kamati huru inayoongozwa na Prof. Penina Mlama, mwaka huu washindani walijitokeza kwa wingi katika nyanja nne kuu ambazo ni riwaya, hadithi za watoto, tamthilia na ushairi."amesema Prof.Mkenda

Prof. Mkenda ameongeza kuwa katika kuenzi uandishi bunifu, hafla ya mwaka huu itapambwa na uwepo wa mgeni rasmi, mshairi mashuhuri duniani Abdilatif Abdalla kutoka Ujerumani, ambaye pia aliwahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 15, jambo linaloipa hafla hiyo uzito wa kipekee kitaifa na kimataifa.

Aidha amesema kuwa  kabla ya hafla hiyo, kutakuwa na mjadala maalum utakaowakutanisha waandishi bunifu wa ndani na nje ya nchi, ukiwahusisha wataalamu mashuhuri akiwemo Dkt. Aida Mutenyo kutoka Uganda na Ferdinand Ndahayo kutoka Rwanda.

Akizungumzia mafanikio ya tuzo hizo, Waziri Mkenda amesema tangu kuanzishwa kwake, jumla ya Watanzania 27 wamefanikiwa kushinda katika makundi mbalimbali, huku Serikali ikiwekeza takribani shilingi milioni 800 kwa ajili ya uchapishaji wa vitabu vilivyoshinda na kusambazwa katika shule za Tanzania Bara na Zanzibar ili kuhamasisha utamaduni wa kusoma.

Prof.Mkenda amebainisha kuwa tuzo hizo pia zimekuwa zikivutia Watanzania waishio nje ya nchi pamoja na washiriki kutoka mataifa mbalimbali, hali inayoonyesha kukua kwa hadhi ya tuzo hizo kimataifa.

"Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi na kuwekeza katika kukuza sekta ya fasihi na uandishi bunifu nchini."amesisitiza Prof.Mkenda

Hata hivyo Waziri Mkenda ameipongeza kamati huru ya tuzo chini ya uongozi wa Prof. Penina Mlama kwa kusimamia mchakato wa upatikanaji wa washindi kwa weledi, haki na uwazi.

Pia Waziri Mkenda amewaalika wananchi wote kushiriki katika hafla hiyo itakayoanza saa nane mchana, akisema kuwa mbali na kutangazwa kwa washindi, pia kutakuwa na burudani ya kazi za kibunifu pamoja na majadiliano yatakayochochea maendeleo ya fasihi nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2026,Prof. Penina Mlama,amesema kuwa mwitikio wa washiriki umekuwa mkubwa na unaonyesha kukua kwa tasnia ya uandishi bunifu, akibainisha kuwa washindi watatu bora kwa kila kipengele watapata zawadi ya fedha taslimu pamoja na fursa ya kuchapishiwa kazi zao.

Post a Comment

Previous Post Next Post