" Yanga Yaisambaratisha Pamba Jiji FC 3-0

Yanga Yaisambaratisha Pamba Jiji FC 3-0


Mabigwa Watetezi Ligi Kuu Tanzanka Bara Yanga SC imeendeleza ubabe baada ya kuichapa Pamba Jiji mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa leo Aprili 8, 2026 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mabao ya Yanga SC yaliyofungwa na Mudathir Yahya mawili na Maxi Nzengeli moja na kutanua rekodi ya mabingwa hao, huku ikiivunja rekodi ya wenyeji wao ambao waliokuwa hawajapoteza mchezo wowote nyumbani msimu huu.

Ushindi huo unakuwa wa 13 kwa Yanga katika Ligi Kuu Bara na kuifanya kuendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 44, ikicheza michezo 18, ikiiachia Simba itakayokuwa uwanjani kesho dhidi ya TRA United iliyoko nafasi ya pili, kuendelea kuwafukuza ingawa wekundu hao wana michezo miwili pungufu.

Haikuwa ngumu Yanga kupata ushindi huo ambapo ilimaliza dakika 45 za kwanza ikiongoza kwa mabao 2-0 yakifungwa na kiungo Mudathir Yahaya dakika ya 8 na 33 yakitosha kuilainisha mechi hiyo.

Mabao hayo mawili yamemfanya Mudathir kuongoza kwa ufungaji kwenye klabu yake akifikisha saba akiwashusha chini washambuliaji wa timu hiyo, Prince Dube na Laurindo Aurellio ‘Depu’ wenye mabao sita kila mmoja.

Kipindi cha pili Yanga iliendeleza moto wake ikipata bao la tatu kupitia kwa kiungo mwingine Maxi Nzengeli na kuipoteza zaidi Pamba Jiji.

Yanga imeendelea kutanua rekodi yake ya kutopoteza mechi kwenye ligi, ikifikisha michezo 38 bila kupoteza ambapo mara ya mwisho kupoteza ilikuwa Novemba 7, 2024 ilipopoteza nyumbani kwa mabao 3-1 dhidi ya TRA United wakati huo ikiitwa Tabora United.

Kabla ya mchezo huo wa leo, Pamba jiji ilikuwa haijapoteza nyumbani msimu huu katika mechi tisa ikishinda tano na sare nne, lakini kipigo hicho cha Yanga ikawatibulia na kupoteza kwa mara ya kwanza.

Yanga iliondoka uwanjani kwa mchezo wa pili mfululizo bila wavu wake kutikiswa ikitumia makipa wawili tofauti tangu kusimamishwa kwa Djigui Diarra anayetumikia adhabu ya kukosa mechi tatu, akibakisha moja kwenye adhabu yake.

Yanga leo golini alikuwa kipa Hussein Masalanga ambaye alipata klinshiti yake ya kwanza kwenye mchezo wake wa kwanza Ligi Kuu Bara akiwa na Yanga. Mchezo uliopita kipa alikuwa Aboutwalib Mshery ambaye hakuonekana uwanjani wala benchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post