" JUMLA YA MIRADI 99 YA BIASHARA YA KABONI YASAJILIWA NCHINI TANZANIA

JUMLA YA MIRADI 99 YA BIASHARA YA KABONI YASAJILIWA NCHINI TANZANIA

 Jumla ya miradi 99 ya biashara ya kaboni imesajiliwa nchini tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Biashara ya Kaboni (NCMC) Machi 2025, hatua inayoonesha kasi ya Tanzania katika kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia uchumi wa kijani.

Hayo yameelezwa Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa NCMC, Dk. Deo Shirima, wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu biashara ya kaboni, ambapo alibainisha kuwa baadhi ya miradi tayari imeanza kuleta matokeo chanya ya utekelezaji.

Dk. Shirima alisema kati ya miradi hiyo, kampuni nane zimeanza rasmi utekelezaji na tayari zimeanza kunufaika kwa kupokea fedha kutoka serikalini, kufuatia hatua zao za kuhifadhi na kuendeleza miradi ya kaboni.

Alifafanua kuwa biashara ya kaboni inalenga kutoa motisha kwa shughuli mbalimbali zinazochangia kupunguza au kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kuimarisha mifumo endelevu ya usimamizi wa mazingira katika sekta za kiuchumi na kijamii.

Alitaja baadhi ya maeneo yanayohusika katika biashara hiyo kuwa ni usimamizi bora wa taka, kilimo endelevu kinacholinda udongo na uoto wa asili, uhifadhi wa misitu, matumizi ya nishati mbadala kama umeme wa jua, pamoja na usafiri endelevu unaopunguza utegemezi wa nishati za mafuta.

“Biashara ya kaboni inaweza kufanywa na kampuni, taasisi au mtu binafsi kupitia shughuli mbalimbali za uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali. Lengo kuu ni kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi hayaathiri mazingira,” alisema Dk. Shirima.

Aliongeza kuwa shughuli za kila siku za binadamu na maendeleo ya kiuchumi zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira, hali inayochochea ongezeko la athari za mabadiliko ya tabianchi duniani.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo, alisema serikali inatarajia wanahabari kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu fursa na umuhimu wa biashara ya kaboni nchini.

Alibainisha kuwa Tanzania inatumia mikakati miwili mikuu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo ni matumizi ya nishati mbadala na kuimarisha uwezo wa mazingira kustahimili athari za mabadiliko hayo.

“Biashara ya kaboni inatoa fursa muhimu ya kiuchumi kwa wananchi, hivyo shughuli za uhifadhi kama upandaji miti na utunzaji wa misitu sasa zinaweza kuwa chanzo cha kipato badala ya kuwa mzigo pekee,” alisema Kwagilwa.

Aliongeza kuwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inalenga kujenga uchumi shindani, kuboresha huduma kwa wananchi na kuhakikisha uendelevu wa mazingira, ambapo biashara ya kaboni ni nyenzo muhimu ya kufanikisha malengo hayo.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa NCMC, Kathryn Kigaraba, alisema kituo hicho kitaendelea kuratibu na kusimamia biashara ya kaboni ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa zilizopo katika masoko ya kimataifa ya kaboni.

Alisisitiza kuwa vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa, uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya kaboni nchini.

“Tunategemea wanahabari kuwa daraja muhimu la kusambaza taarifa sahihi na za wakati ili wananchi waelewe namna wanavyoweza kunufaika na sekta hii inayokua kwa kasi,” alisema Kigaraba.       

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post