" KAMPUNI 550 KUTOKA ULAYA NA AFRIKA KUSHIRIKI MAONYESHO YA UTALII KARIBU KILIFAIR MWAKA HUU

KAMPUNI 550 KUTOKA ULAYA NA AFRIKA KUSHIRIKI MAONYESHO YA UTALII KARIBU KILIFAIR MWAKA HUU

Na Seif Mangwangi, Arusha 

ZAIDI ya kampuni 550 zinazojishughulisha na utalii kutoka bara la Afrika na Ulaya zimejisajili kushiriki kwenye maonyesho ya Kimataifa ya utalii maarufu kama Karibu KiliFair kwa msimu wa mwaka huu 2026.


Akizungumza kwenye mkutano wa wadau kuelekea kwenye ufunguzi wa maonyesho hayo ya utalii Kimataifa, Mkurugenzi mwenza wa Karibu KiliFair, Dominic Shoo, amesema waonyeshaji hao wanatoka katika nchi 14 za Afrika na Ulaya, ambapo pia kutakuwepo na mawakala wa utalii 1,000, waendeshaji wa utalii kutoka nchi zaidi ya 40, na wadau na wapenda utalii 15,000.

Shoo amesema washiriki wa maonyesho hayo wamekuwa wakiongezeka Kila mwaka kutokana na utalii kukua na kuwa nguzo ya uchumi wa Tanzania.

Amesema kwa mujibu wa makadirio ya Baraza la Utalii Duniani (WTTC, 2024/2025), mchango huo huongezeka hadi karibu asilimia 17, pale athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zinapojumuishwa .


"Utalii umekuwa moja ya nguzo kuu za uchumi wa Tanzania tangu uhuru, kwa sasa, sekta hii inachangia takribani dola za Marekani bilioni 6.5, sawa na karibu asilimia 10 ya Pato la Taifa (GDP),”amesema na kuongeza:

“Hii inaonesha umuhimu mkubwa wa sekta hii katika kuchochea ukuaji wa uchumi, kusaidia maisha ya wananchi na kupunguza umaskini. Hali ya sasa katika sekta ya utalii ni nzuri sana, na nafasi za uhifadhi kuanzia Mei 2025 zinaonekana kuongezeka kwa kiwango kikubwa katika hoteli nyingi, lodge na kampuni za utalii".

Kwa upande wake Mkurugenzi mwenza wa maonyesho hayo,Tom Kunkler, amesema licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo ya kipekee zaidi duniani kwa utalii, bado fursa za biashara hazijaunganishwa kikamilifu kupitia vivutio vya kipekee vya wanyamapori na asili.


Kwa mujibu wa Kunkler, mapato ya ziada yanayotokana na programu za kimataifa za tabianchi, yanaweza kuwa fursa ya kupunguza changamoto za kifedha za serikali, huku yakichangia pia kuboresha maisha ya jamii za wenyeji.

Kunkler amesema pamoja na changamoto zilizopo bado Tanzania inayo nafasi nzuri ya kunufaika na fursa za uwekezaji zinazolenga kuhifadhi na kuimarisha mazingira ikiwemo utoaji wa huduma mbalimbali za mifumo ikolojia, ikiwamo ufyonzaji wa kaboni na manufaa ya ziada ya bioanuwai, ambayo hayajapangiwa bei kwa ufanisi na mara nyingi hayazalishi faida yoyote ya kifedha.

Maonyesho hayo ya kimataifa ya utalii yanatarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Juni 4 hadi 7 mwaka huu, yakihusisha mataifa ya Ujerumani, Tanzania, Uganda, Nigeria, Ghana, South Afrika, Uturuki, Kenya, Zimbabwe, Zambia, Ethiopia, Rwanda na Zanzibar.



Post a Comment

Previous Post Next Post