Na Mwandishi wetu Dodoma
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imefichua kasoro nzito katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa mabweni ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaigwa wilayani Kongwa, ambapo baadhi ya kazi zimeonekana kutotekelezwa kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mikataba ya Serikali.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari leo jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli za TAKUKURU kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Christopher Myava, amesema taasisi hiyo imebaini matumizi ya nyavu kwenye madirisha na sehemu za hewa za milango badala ya vioo vilivyotakiwa kuwekwa kwa mujibu wa ramani ya ujenzi.
Amesema uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU umeonesha pia kuwa baadhi ya vyoo vya mabweni hayo havikuwekewa masinki kama ilivyoelekezwa kwenye michoro ya mradi, huku kuta zikikosa vigae vilivyopangwa kufungwa kwa mujibu wa makubaliano ya utekelezaji wa kazi hiyo.
“Tumebaini tofauti kubwa kati ya kazi iliyotekelezwa na maelekezo yaliyopo kwenye mkataba wa mradi. Haya ni mambo ambayo yanaathiri ubora wa miradi pamoja na thamani ya fedha za Serikali,” amesema Myava.
Mbali na dosari hizo, TAKUKURU imeeleza kuwa baadhi ya vitasa vilivyowekwa kwenye mabweni hayo havifanani na vile vilivyoainishwa kwenye mkataba, huku baadhi ya vifaa vya ujenzi ikiwemo matofali na mabati vikidaiwa kutowasilishwa maabara kwa ajili ya kupimwa ubora wake kabla ya kutumika kwenye mradi.
Katika hatua nyingine, Myava amesema taasisi hiyo imefanikiwa kubaini mapungufu katika jumla ya miradi 36 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 156.4 kupitia operesheni za ufuatiliaji zilizofanywa katika sekta mbalimbali mkoani Dodoma.
Amesema TAKUKURU itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha fedha za umma zinaleta matokeo yaliyokusudiwa na wananchi wanapata huduma bora kutokana na uwekezaji wa Serikali.
“Lengo letu ni kuona miradi yote inakamilika kwa viwango vinavyostahili na kuhakikisha hakuna mianya ya ubadhirifu wa fedha za umma,” ameongeza.
Baada ya kubaini dosari hizo, wahusika wa miradi hiyo wamepewa maelekezo ya kurekebisha mapungufu yote yaliyojitokeza ili miradi hiyo iweze kukidhi viwango vya kitaalamu pamoja na thamani ya fedha zilizotumika.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment