Na Lydia Lugakila-Misalaba Media
Mbeya
Mchungaji Thobias Tambikeni wa Tanzania Assemblies of God (TAG)Forest ya Kwanza jijini Mbeya, amesema waumini wanapaswa kumpa Mungu nafasi ndani ya mioyo yao ili waweze kupata majibu kupitia imani.
Akihubiri kanisani, mchungaji huyo amesema kuwa wakati mwingine waumini hushiriki ibadani lakini hawampi Mungu nafasi ya kutenda kazi katika maisha yao kwa sababu mioyo yao huwa finyu katika kuamini.
Amesema njia rahisi ya kupata majibu kutoka kwa Mungu ni kuwa na imani na kutokata tamaa, kwani Mungu hutumia mapambano ya maisha kuwaletea waumini utukufu mkubwa.
“Kwa mtu anayempa Mungu nafasi ya kiroho hata wakati wa misukosuko, Mungu hutenda kazi katika maisha yake hivyo tunapaswa kumuachia Mungu nafasi ili atupiganie, kwa kuwa hatuna wa kumtegemea zaidi ya Yesu Kristo,” alisema Mtumishi huyo wa Mungu.
Aidha, amewakumbusha waumini kuwa siku za mwisho zinahitaji watu kujishughulisha zaidi na mambo ya msingi ya kiroho ili kumruhusu Mungu kuondoa vikwazo katika maisha yao.
Kuhusu fedha, mchungaji huyo amesema pesa hazipaswi kuwatawala watu bali wanapaswa kuzitawala wao, akionya kuwa tamaa ya fedha inaweza kumfanya mtu kuwa mwongo na kuacha haki.
Pia alitaja baadhi ya tabia zinazowafanya waumini kukosa majibu kutoka kwa Mungu kuwa ni kiburi, kujikweza, kulaumu na kunung’unika kupita kiasi.
“Watu wenye tabia ya kuwatukana na kutowaheshimu wazazi hawawezi kusonga mbele nasisitiza vinywa vyetu vitumike kwa maombi na maneno mema, si kwa lugha mbaya,” alisisitiza.
Akiwaasa vijana, amesema baadhi yao wamekuwa wakiwapuuza wazazi wao badala ya kuwaheshimu, huku akieleza kuwa kuwaheshimu wazazi ni amri ya kwanza yenye ahadi ya baraka.
Vilevile, amezitaka familia zinazokumbwa na migogoro kujitahidi kutatua changamoto zao kwa njia ya amani ili kudumisha upendo na kumcha Mungu.
Amemalizia kwa kusema kuwa mtu anayempa Mungu nafasi hupata majibu, na hata anayepitia magumu anaweza kuinuka tena anapokutana na watu wenye hofu ya Mungu.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment