" UFUKUNYUNGU FC WATINGA HATUA INAYOFUATA LICHA YA KUPOTEZA, MWASENGE FC YAONDOKA KISHUJAA NIACHEKONA CUP 2026

UFUKUNYUNGU FC WATINGA HATUA INAYOFUATA LICHA YA KUPOTEZA, MWASENGE FC YAONDOKA KISHUJAA NIACHEKONA CUP 2026

Na Mapuli Kitina Misalaba

Timu ya UFUKUNYUNGU FC kutoka kata ya Ngokolo mjini Shinyanga imefanikiwa kusonga mbele katika mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 licha ya kupoteza mchezo wa leo kwa bao 1-0 dhidi ya MWASENGE FC kutoka kata ya Salawe.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ndani ya uwanja wa Mwabenda kata ya Solwa, MWASENGE FC walifanikiwa kupata ushindi wa bao moja lakini matokeo hayo hayakutosha kuiondoa UFUKUNYUNGU FC kutokana na hesabu ya jumla ya mabao katika michezo miwili ya mtoano.

Ikumbukwe kuwa katika mchezo wa kwanza uliochezwa kati ya timu hizo, UFUKUNYUNGU FC waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya MWASENGE FC, hali iliyowalazimu MWASENGE FC kuhitaji ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa leo ili waweze kufuzu hatua inayofuata ya mashindano hayo.

Kutokana na ushindi wa leo wa bao 1-0, MWASENGE FC wamejikuta wakiondolewa rasmi katika mashindano hayo huku UFUKUNYUNGU FC wakifanikiwa kuendelea mbele kwa jumla ya mabao 2-1.

Kutokana na ushindi huo wa jumla ya mabao 2-1, timu ya UFUKUNYUNGU FC sasa itakutana na HOME BOYS katika hatua inayofuata ya mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu zote mbili kuonesha kiwango kizuri katika michezo yao ya awali.

Baada ya mchezo huo, viongozi wa MWASENGE FC wamemshukuru mwandaaji wa mashindano hayo Paul Daud Augustino kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika mashindano hayo huku wakiahidi kurejea kwa nguvu zaidi katika mashindano yajayo.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Mashindano Sambayi Jilya ametangaza ratiba ya mchezo wa kesho ambapo timu ya MWANDUTU FC itamenyana na DUARA FC katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ndani ya mashindano hayo.

Aidha amewahimiza wananchi pamoja na mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa Mwabenda kuendelea kushuhudia burudani ya soka pamoja na vipaji vya vijana vinavyoendelea kuibuliwa kupitia mashindano hayo.

Mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 yameandaliwa na Paul Daud Augustino kupitia ufadhili wa shirika la Lushu Foundation kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana, kukuza michezo pamoja na kuimarisha mshikamano wa jamii kupitia soka.

Kwa huduma za ushereheshaji wa shughuli mbalimbali, matangazo pamoja na burudani unaweza kuwasiliana na Paul Daud Augustino kupitia namba 0757 267 738.

Timu ya Mwasenge FC



 

Post a Comment

Previous Post Next Post