" KAMATI YA UTEKELEZAJI JUMUIYA YA WAZAZI MPANDA YAKAMILISHA MAANDALIZI YA BARAZA LA WILAYA

KAMATI YA UTEKELEZAJI JUMUIYA YA WAZAZI MPANDA YAKAMILISHA MAANDALIZI YA BARAZA LA WILAYA

Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda imefanya kikao chake Juni 24, 2026 kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na uhai wa jumuiya hiyo pamoja na kufanya maandalizi ya Baraza la Wazazi la Wilaya litakalofanyika Juni 25, 2026.

Kikao hicho kilijadili kwa kina suala la kuimarisha uhai wa Jumuiya ya Wazazi, ambapo wajumbe walisisitiza umuhimu wa viongozi na wanachama katika ngazi zote kuendelea kulipia ada za uanachama ili kuhakikisha jumuiya inaendelea kuwa hai na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Aidha, wajumbe walijadili mikakati ya kuongeza idadi ya wanachama kupitia kampeni ya usajili katika matawi na kata mbalimbali za Wilaya ya Mpanda. Kikao hicho kilikubaliana kuwa viongozi wa jumuiya kwa kushirikiana na maafisa wa TEHAMA watembelee maeneo mbalimbali kutoa elimu kuhusu namna ya kujiunga na jumuiya na kulipia ada kwa njia za kidijitali, ikiwemo simu, mawakala na benki.

Katika kikao hicho, wajumbe pia walijadili hatma ya Shule ya Sekondari na Ufundi Milala iliyopo Kijiji cha Milala, Kata ya Misunkumilo, ambayo imekuwa haifanyi kazi kwa kipindi cha takribani miaka mitano. Wajumbe walieleza kuwa shule hiyo ni mali ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda na kuna haja ya kuendelezwa ili iweze kutoa mafunzo mbalimbali ya elimu na ufundi kwa vijana.

Kamati hiyo ilibaini kuwa changamoto kubwa inayokabili shule hiyo ni ukosefu wa hati miliki ya eneo pamoja na gharama za upimaji wa eneo hilo zinazokadiriwa kufikia shilingi milioni 2.3. Wajumbe walisisitiza kuwa hakuna mgogoro wowote kati ya shule hiyo na taasisi nyingine kama ambavyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakidai, na kwamba juhudi zinaendelea kufanyika ili kupata hati miliki na kuendeleza shule hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda imewaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kusaidia juhudi za kuendeleza shule hiyo kwa manufaa ya jamii na kizazi kijacho.

Kikao hicho pia kilijadili miradi mbalimbali ya kiuchumi inayolenga kuongeza uwezo wa kifedha wa jumuiya. Wajumbe walihimizwa kubuni na kuanzisha miradi katika ngazi za matawi na kata ili kuongeza vyanzo vya mapato na kuifanya jumuiya kujitegemea zaidi.

Kwa upande mwingine, kamati ilipokea taarifa ya tathmini ya Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi yaliyofanyika Mei 7, 2026 katika Hospitali ya Halmashauri ya Nsimbo, Kata ya Mtapenda. Wajumbe walieleza kuridhishwa na mafanikio ya maadhimisho hayo yaliyohusisha utoaji wa misaada kwa wagonjwa pamoja na upandaji wa miti ya matunda na kivuli.

Maadhimisho hayo yaliongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Katavi, Ndugu Evarist Simon Mnyele, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika maandalizi ya Baraza la Wazazi Wilaya ya Mpanda litakalofanyika Juni 25, 2026, kamati ilisisitiza umuhimu wa kutekeleza majukumu ya jumuiya kwa mujibu wa katiba, kanuni na maelekezo ya chama. Pia ilipendekeza kuendelea na ziara za viongozi katika matawi na kata kwa lengo la kutoa elimu kuhusu malezi, mazingira na kuimarisha uhai wa jumuiya.

Wajumbe walijadili pia maandalizi ya ushiriki wa Wilaya ya Mpanda katika Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi Kitaifa yatakayofanyika Mkoani Mwanza kuanzia Juni 30 hadi Julai 4, 2026. Kamati ilieleza umuhimu wa wanachama kushiriki maadhimisho hayo ili kuimarisha mshikamano na kubadilishana uzoefu na wanachama kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda, Ndugu Jimotoli Jilala Maduka, aliwataka viongozi na wanachama kuendelea kudumisha umoja na mshikamano huku wakihamasisha wanachama wengi zaidi kushiriki katika maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Wazazi yatakayofanyika Mwanza.

Amesema umoja na mshikamano ni msingi muhimu wa mafanikio ya jumuiya na Chama Cha Mapinduzi, hivyo kila mwanachama ana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali zinazolenga kuimarisha maendeleo ya jumuiya na jamii kwa ujumla.

 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Ndugu Pius M. Buzumalle, akifungua kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda leo Juni 24, 2026, saa 4:30 asubuhi, kilicholenga kufanya maandalizi ya Baraza la Wazazi Wilaya ya Mpanda litakalofanyika Juni 25, 2026. Katika ufunguzi wake, aliwataka wajumbe kuwa watulivu, kufuatilia agenda za kikao na kutoa michango yenye kujenga kwa maendeleo ya Jumuiya.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

 

Post a Comment

Previous Post Next Post