" REA ZAMBIA YAPONGEZA UBORA WA MIRADI YA UMEME VIJIJINI TANZANIA

REA ZAMBIA YAPONGEZA UBORA WA MIRADI YA UMEME VIJIJINI TANZANIA

Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA) kutoka nchini Zambia yapongeza utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Pongezi hizo zimetolewa leo Juni 24, 2026 na Mtendaji Mkuu wa REA Zambia, Mhandisi Alex Mbumba wakati wa ziara ya viongozi hao walipotembelea miradi ya umeme vijijini katika Kijiji cha Vikonje Mkoani Dodoma.

“Tumekuja Tanzania kujifunza na kujionea namna miradi ya umeme vijijini inavyotekelezwa baada ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa ya kufikisha umeme kwenye vijiji vyake vyote.

Tumekuwa na vikao na uongozi wa REA Tanzania toka tulivyowasili nchini kwa ajili ya kujifunza. Leo tumekuja kuona miradi ya umeme inavyotekelezwa na namna ilivyonufaisha na kuboresha maisha ya wananchi vijijini. Tumeona REA Tanzania inavyotekeleza miradi yake kwa ubora na viwango vya Kimataifa,” amesema Mhandisi Mbumba huku akiwahamasisha wananchi kutumia umeme kujiletea maendeleo.

Kwa upande wake Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya kupeleka Umeme Vijijini kutoka REA Tanzania, Mhandisi Deogratius Nagu amesema kuwa ujio wa ugeni huo kutoka REA Zambia ni ishara ya kutambuliwa kwa mafanikio yaliyofikiwa nchini katika kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi vijijini.

“Tanzania ni moja kati ya nchi chache Barani Afrika zilizofanikiwa kufikisha umeme katika vijiji vyake vyote, hivyo basi wenzetu wa Zambia wameona waje wajifunze ni kwa namna gani tumefanikiwa kutekeleza miradi yetu na kufikia mafanikio ya kufikisha umeme vijiji vyote vya Tanzania Bara,” amesema Mhandisi Nagu.

Post a Comment

Previous Post Next Post