" KATAMBI ONYA WANAOTAKA KUICHOMA MOTO NCHI KWA MKUMBO WA MAANDAMANO NA UCHOCHEZI MITANDAONI

KATAMBI ONYA WANAOTAKA KUICHOMA MOTO NCHI KWA MKUMBO WA MAANDAMANO NA UCHOCHEZI MITANDAONI

  


Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametoa onyo kali kwa wananchi wanaofuata mkumbo wa kushawishiwa kuvunja sheria na amani ya taifa, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia mtu au kikundi chochote kinacholenga kuichoma moto nchi kwa maslahi binafsi.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa na waumini wa Msikiti wa Mukadam uliopo Kata ya Chang’ombe, Wilaya ya Dodoma Mjini wakati wa mashindano ya Qur’an na harambee ya ujenzi wa msikiti huo, Katambi alisema kuwa amani na umoja wa nchi ndio misingi mikuu ya maendeleo ambayo haipaswi kuchezewa hata kidogo.

Waziri Katambi alifafanua kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la kauli za uchochezi na kibaguzi zinazolenga kudhoofisha Muungano na kuleta mifarakano kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kisiasa, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi na ustawi wa jamii.

Kuhusu mipango ya siri na wazi ya baadhi ya watu wanaoandaa na kuhamasisha maandamano haramu yanayopangwa kufanyika Julai 7, 2026, Katambi alipiga marufuku vitendo hivyo na kubainisha kuwa hatua hizo zisizo za kisheria zina lengo la kuingiza taifa kwenye machafuko, hivyo amewataka vijana kuwa mstari wa mbele kukataa katakata kushawishiwa au kutumiwa kama chambo cha kuvunja sheria.

Aliwakumbusha wananchi kuwa kuishi kwa kufuata mikumbo ya kisiasa bila kutafakari madhara yake kunaweza kubomoa taifa kwa sekunde chache, wakati ujenzi wa amani iliyopo umegharimu miaka mingi ya jasho na uzalendo wa hali ya juu.

Waziri Katambi alihitimisha kwa kutoa agizo madhubuti kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini kote kuendelea kuchukua hatua kali na za haraka bila muhali kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na uchochezi, huku akitoa rai kwa kila Mtanzania kuheshimu maelekezo ya mamlaka ili kudumisha utulivu na maendeleo ya kiuchumi.

Post a Comment

Previous Post Next Post