" KIMANDAGULI FC YAITOA KASHISHI FC KWA PENATI, YATINGA TIMU 12 BORA NIACHEKONA CUP 2026

KIMANDAGULI FC YAITOA KASHISHI FC KWA PENATI, YATINGA TIMU 12 BORA NIACHEKONA CUP 2026


Na Mapuli Kitina Misalaba

Timu ya Kimandaguli FC imefanikiwa kutinga hatua inayofuata ya mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 6-5 dhidi ya Kashishi FC katika mchezo wa marudiano uliochezwa leo Juni 4, 2026 katika uwanja wa Mwabenda, Kata ya Solwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Kimandaguli FC iliingia uwanjani ikiwa na faida ya ushindi wa mabao 3-1 walioupata katika mchezo wa kwanza, lakini Kashishi FC walionesha dhamira ya kusaka ushindi na kufanikiwa kushinda mabao 2-0 ndani ya dakika 90 za mchezo.

Matokeo hayo yaliifanya jumla ya mabao katika michezo yote miwili kuwa sare ya 3-3, hali iliyolazimu mshindi kupatikana kwa mikwaju ya penati kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo.

Katika hatua hiyo ya penati, Kimandaguli FC walionesha utulivu na umakini mkubwa kwa kufanikiwa kushinda kwa penati 6-5 na hivyo kuendelea na safari yao ya kuwania ubingwa wa NIACHEKONA CUP 2026, huku Kashishi FC wakihitimisha safari yao katika mashindano hayo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Katibu wa Kamati ya Mashindano Sambayi Jilya ametangaza kuwa mchezo wa kesho utawakutanisha Mwakitolyo No. 6 na Isenengeja FC katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Ameendelea kuwakaribisha wananchi, wadau wa michezo na mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa Mwabenda ili kuendelea kushuhudia vipaji vya vijana na burudani ya michezo inayotolewa kupitia mashindano hayo.

Mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 yameandaliwa na mdau wa michezo Paul Daud Augustino maarufu MC NIACHEKONA kwa ufadhili wa shirika la Lushu Foundation, yakiwa na lengo la kuibua vipaji vya vijana, kuimarisha amani na kukuza michezo katika jamii.

Kwa mawasiliano ya huduma za ushereheshaji wa shughuli mbalimbali, matangazo na matukio ya kijamii, MC NIACHEKONA anapatikana kupitia namba 0757 267 738.

Kikosi cha Kimandaguli FC na kocha wa timu.



 

Post a Comment

Previous Post Next Post