NA MWANDISHI WETU, NOEL RUKANUGA
Katika michuano ya Kombe la Dunia 2026, huenda hakuna kundi lililoibua mvuto mkubwa kama Kundi C. Baada ya kila timu kucheza mechi mbili, Brazil na Morocco zina pointi nne kila moja, Scotland ina pointi tatu, huku Haiti ikisalia bila pointi.
Kwa mtazamo wa haraka, unaweza kudhani Brazil na Morocco tayari zimeweka mguu mmoja katika hatua ya 32 Bora. Hata hivyo, ukiangalia kwa undani zaidi, utaona kuwa hakuna timu iliyojihakikishia kufuzu.

Ili ni kundi lenye simulizi nyingi kwa wakati mmoja. Brazil inapambana kurejesha hadhi yake ya kuwa miongoni mwa mataifa makubwa ya soka duniani. Morocco inataka kuthibitisha kuwa mafanikio yake ya miaka ya karibuni hayakuwa ya bahati nasibu.
Scotland inatafuta kurejea katika ramani ya soka la dunia, huku Haiti, licha ya kupoteza mechi zake zote mbili, bado ikiwa na uwezo wa kuathiri hatima ya wapinzani wake.
Kilichoongeza mvuto wa kundi hili ni kwamba hakuna timu iliyoonyesha ubabe wa wazi dhidi ya washindani wote baada ya michezo miwili ya mwanzo.
Brazil ilianza kwa sare ya mabao 1-1 dhidi ya Morocco kabla ya kuichapa Haiti mabao 3-0. Morocco nayo ilitoka sare na Brazil kisha ikaifunga Scotland kwa bao 1-0.
Kwa upande mwingine, Scotland iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Haiti lakini ikapoteza mbele ya Morocco. Matokeo hayo yanaonyesha tofauti ya viwango si kubwa kama wengi walivyotarajia kabla ya mashindano kuanza.
Kama kuna timu iliyothibitisha kuwa na jambo la kipekee katika kundi hili, basi ni Morocco.
Baada ya kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022, kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu iwapo mafanikio hayo yangekuwa mwanzo wa zama mpya katika soka la taifa hilo.
Kilichoonekana katika mechi mbili za kwanza kinaashiria kuwa Wamorocco bado wanaendelea kupiga hatua.
Sare dhidi ya Brazil iliwaongezea kujiamini, huku ushindi dhidi ya Scotland ukionyesha uwezo wao wa kushinda hata wanapobeba jukumu la kutawala mchezo.
Tofauti na miaka ya nyuma ambapo timu nyingi za Afrika zilijulikana zaidi kwa nguvu na kasi, Morocco ya sasa inaonyesha utulivu wa kiufundi, umiliki mzuri wa mpira na nidhamu ya kimfumo.
Ndiyo maana mchezo wao wa mwisho dhidi ya Haiti una umuhimu mkubwa. Ushindi utawafikisha pointi saba, idadi ambayo mara nyingi hutosha kumaliza katika nafasi mbili za juu za kundi.
Brazil inaongoza kundi kwa tofauti ya mabao, lakini ukweli ni kwamba bado haijatoa ujumbe wa kutisha kwa washindani wake.
Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Haiti ulidhihirisha ubora wa kikosi chao, lakini kipimo halisi kilikuwa mchezo dhidi ya Morocco ambapo walionekana kupata wakati mgumu.
Jambo linaloweza kuwapa wasiwasi mashabiki wa Brazil ni kwamba katika soka la kisasa, mafanikio makubwa hayategemei vipaji pekee bali pia uimara wa mfumo wa mchezo. Hadi sasa, Morocco imeonekana kuwa na uthabiti mkubwa katika eneo hilo.
Kutokana na hali hiyo, mechi ya mwisho dhidi ya Scotland inaweza kuwa mtihani mgumu zaidi kuliko wengi wanavyotarajia. Scotland itaingia uwanjani ikijua ushindi unaweza kuipeleka moja kwa moja hatua inayofuata.
Ikiwa kuna timu inayoweza kuvuruga hesabu zote za kundi hili, basi ni Scotland.
Tayari ina pointi tatu, hivyo ushindi dhidi ya Brazil utaifikisha pointi sita na kuiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu.
Hata sare inaweza kuendelea kuipa matumaini, kutegemea matokeo ya Morocco dhidi ya Haiti pamoja na hesabu za timu bora zitakazomaliza katika nafasi ya tatu.
Changamoto kubwa kwa Scotland ni kukutana na timu yenye uzoefu mkubwa wa mashindano makubwa. Brazil imezoea kucheza mechi za presha ya kiwango hiki kuliko karibu taifa lolote duniani.
Hata hivyo, shinikizo linaweza pia kuwa upande wa Brazil. Wabrazil wanajua kuwa kupoteza kunaweza kuwashusha hadi nafasi ya tatu au hata kuhatarisha safari yao ya kufuzu.
Kwa kawaida, timu inayopoteza mechi mbili za mwanzo huonekana kama mshiriki wa kukamilisha ratiba. Hata hivyo, Haiti bado inaweza kuwa na neno la mwisho katika kundi hili.
Ikiifunga Morocco, hesabu zote zitabadilika ghafla. Ingawa hilo linaonekana kuwa gumu kutokana na kiwango ilichoonyesha hadi sasa, historia ya Kombe la Dunia imejaa matokeo yaliyowashangaza wengi.
Mara nyingi timu ambazo tayari zimeonekana kuwa nje ya mashindano hucheza bila presha, jambo linaloweza kuzifanya kuwa hatari zaidi.
Hali rahisi zaidi ni Brazil na Morocco kushinda mechi zao za mwisho. Matokeo hayo yatazifikisha pointi saba na kuzihakikishia kufuzu moja kwa moja.
Lakini Scotland ikiifunga Brazil, sura ya kundi itabadilika kabisa. Brazil inaweza kujikuta ikitegemea tofauti ya mabao, huku Morocco ikipambana kumaliza kileleni au katika nafasi ya pili kulingana na matokeo yake.
Iwapo Brazil na Scotland zitatoka sare, Scotland itafikisha pointi nne na kuanza kuhesabu nafasi yake miongoni mwa timu bora zitakazomaliza nafasi ya tatu.
Kwa sasa, Haiti inaonekana kubaki nyuma, lakini kati ya Brazil, Morocco na Scotland kila timu bado ina sababu ya kuamini.
Brazil ina historia na ubora wa kikosi, Morocco ina mfumo thabiti na kujiamini. Scotland ina matumaini pamoja na hamasa ya kufanya makubwa.
Ndiyo maana Kundi C limekuwa miongoni mwa makundi yanayovutia zaidi katika Kombe la Dunia 2026, na mechi za mwisho zinaweza kubadilisha kila kitu kwa muda mfupi.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment